Trump, Putin kuzungumzia Ukraine leo
18 Machi 2025Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la anga la Kiev, usiku wa kuamkia Jumanne (18 Machi) Urusi ilirusha droni 137 za mashambulizi, ambapo 63 kati yake zilidunguliwa na mfumo wa anga wa Ukraine na nyengine 64 "kupotea njia" bila ya kusababisha madhara yoyote.
Kwa kutumia msamiati wa kupotea njia, jeshi hilo la anga lilimaanisha kuwa droni hizo zilidukuliwa kieletroniki na kuongozwa kuelekea mahala kwengine.
Soma zaidi: Marekani na Urusi zakubaliana kumaliza vita Ukraine
Hayo yalijiri wakati Rais Donald Trump wa Marekani alikuwa akitazamiwa kuzungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, katika jitihada za kukomesha vita hivyo vilivyodumu kwa mwaka wa tatu sasa.
Akiandika kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema vipengele vingi vya Makubaliano ya Mwisho vilikuwa vimeshakubalika, ingawa bado kulikuwa na mambo kadhaa yaliyosalia.
"Maelfu ya wanajeshi vijana, na raia wengine, wanauawa. Kila wiki, kuna vifo takribani 2,500 vya wanajeshi wa pande zote, na lazima mauaji haya yamalizike sasa." Aliongeza rais huyo wa Marekani.
Wasiwasi wa Putin
Licha ya Putin kumpongeza Trump kwa juhudi zake za kusaka suluhisho kwenye mzozo wa Ukraine, ambao ulianzishwa na Moscow kwa uvamizi wake wa Februari 2022, kiongozi huyo wa Urusi amekuwa akionesha hadhari kubwa kwenye kulikubali pendekezo la usitishaji mapigano wa siku 30, ambalo Washington imekubaliana na Kiev.
Putin haamini kuwa masharti ya makubaliano hayo yanaweza kutekelezwa, akisisitiza kuwa sababu za vita hivyo lazima ziwekwe wazi ili kupata amani ya kudumu.
Soma zaidi: Trump na Putin kujadiliana kuhusu Ukraine wiki hii
Kwa Urusi, sababu hizo zinajumuisha hakikisho kwamba kamwe Ukraine haitakuwa mwanachama wa muungano wa kijeshi wa mataifa ya Magharibi, NATO.
Ukraine yalegeza kamba
Kwa upande mwengine, Ukraine, ambayo mara kadhaa imekuwa ikionya kwamba kusingewezekana kupatikana kwa suluhisho lolote kwa mzozo huo bila ya kuihusisha Kiev, ilionekana kulegeza msimamo wake.
Waziri wa Mambo ya Kigeni, Andrii Sybiha, alisema kwamba wao si kikwazo kwa makubaliano ya amani na Urusi na kwamba alikuwa anaamini amani ya kudumu ingeliweza kupatikana chini ya uongozi wa Rais Trump wa Marekani.
Soma zaidi: Ukraine na Urusi zaendelea kushambuliana kwa droni
"Sisi sio kikwazo cha kupatikana kwa amani, kwa hakika tunatarajia kauli ya kukubali usitishaji mapigano bila masharti kutoka upande wa Urusi." Alisema waziri huyo wakati akizungumza kwenye kongamano la siasa za kilimwengu mjini New Delhi, India, siku ya Jumanne (Machi 17).
Mazungumzo ya Putin na Trump huenda yakapelekea mkutano wa wawili hao unaoweza kufanyika nchini Saudi Arabia, kama yalivyokuwa mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine, ingawa tarehe rasmi ilikuwa haijatangazwa.