Trump na Zelensky wazungumza kuhusu kumaliza vita Ukraine
20 Machi 2025Katika mazungumzo hayo ya kwanza tangu majibizano yao makali katika ikulu ya White House mnamo Februari 28, Zelensky alimshukuru Trump kwa msaada wa Marekani, na viongozi hao wawili wamekubaliana kutuma katika siku zijazo, wawakilishi huko Saudi Arabia ili kuendeleza mchakato wa amani.
Soma pia: Trump na Putin wakubaliana kutoshambuliwa miundo mbinu ya nishati
Wakati wa mazungumzo hayo yaliyodumu kwa saa nzima, Trump alimueleza Zelenskiy yale aliyoafikiana na rais wa Urusi Vladimir Putin huku rais huyo wa Ukraine akimwomba Trump msaada zaidi wa vifaa vya ulinzi wa anga ili kukabiliana na mashambulizi ya Urusi.
Viongozi hao wawili walijadili pia suala la Marekani kutoa dhamana ya usalama kwa kuchukua udhibiti wa kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia.