Trump na Zelensky wafanya mazungumzo kwa simu
19 Machi 2025Mazungumzo hayo yamefanyika wakati vikosi vya Ukraine na Urusi vikiendelea kushambuliana licha ya Putin na Trump kukubaliana juu ya usitishwaji wa mapigano.
Msemaji wa Zelenskiy, Sergey Nykyforov, amewaambia waandishi habari muda mchache uliopita kwamba Rais Zelenskiy alikuwa kwenye simu na mwenzake wa Marekani Donald Trump.
Akizungumza awali na waandishi habari, Zelenskiy alifahamisha kuwa yeye na Trump wangejadili maelezo ya hatua zinazofauta baada ya majadiliano ya kusitisha vita, akitaja mkutano wa Jeddah, na kueleza kuwa kila kitu kilikubalika, huku akiinyooshea kidole Urusi ambayo alisema haitaki mambo yaende vizuri.
Naibu Mkuu wa Utumishi wa Ikulu ya White House Dan Scavino, pia amesema kupitia mtandao wa kijamii wa X kuwa Trump alikuwa kwenye simu katika ofisi ya Oval.
Soma pia:Trump asema mengi yamekubaliwa kuhusu Ukraine kuelekea simu yake na Putin
Hata hivyo, licha ya makubaliano ya kusitisha mashambulizi ya Urusi kwa muda wa siku 30, bado mapigano yanaendelea. Usiku wa kuamkia leo, Urusi imefanya mashambulizi mengine ya anga dhidi ya miundombinu ya Ukraine, na Rais Zelensky amesisitiza kuwa Marekani inapaswa kuwa na jukumu kubwa katika usimamizi wa makubaliano hayo, hasa katika maeneo ya nishati.
Pamoja na hayo, Zelensky amesema Ukraine itajiandaa kuheshimu makubaliano hayo, lakini ikiwa Urusi haitashambulia tena vituo vya Ukraine, basi nchi yake haitashambulia pia vituo vya Urusi.
Trump na Putin kufanya majadiliano pia
Katika hatua nyingine, mwakilishi maalum wa Marekani, Steve Witkoff, amesema mkutano kati ya Trump na Rais Putin wa Urusi unatarajiwa kufanyika muda wowote, baada ya marais hao kuzungumza na njia ya simu.
Licha ya mapatano ya usitishaji vita kwa muda, Moscow na Kyiv zimeendelea kushtumiana leo kwa kufanya mashambulizi ya anga ambayo yameharibu miundombinu
Katika hatua nyingine, Ujerumani imetangaza kupeleka msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine. Ujerumani ina mpango wa kutoa vifaa vya kijeshi vyenye thamani ya mabilioni ya euro, ikiwa ni sehemu ya msaada wa kiusalama kwa Ukraine mwaka huu na miaka ijayo.
Soma pia:Ujerumani yasema Urusi inacheza mchezo dhidi ya Ukraine
Wakati mzozo unaendelea, wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imebainisha utofauti kati ya maneno ya Urusi na vitendo vyake, hasa katika muktadha wa mashambulizi yake yasiyokoma dhidi ya miundombinu ya kiraia ya Ukraine, licha ya kudai kusitisha mashambulizi.
Wakati Zelensky akizungumza na Trump, jumuiya ya kimataifa inabaki ikielekeza macho yake kwa hatua zinazofuata katika hali inayobaki kuwa tete na inayobadilika.