Trump na Ramaphosa waibua matumaini mapya ya amani DRC
22 Mei 2025Katika mkutano uliofanyika mjini Washington, DC, Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wameeleza kwa pamoja matumaini ya kupatikana kwa suluhisho la kudumu katika mzozo wa muda mrefu kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Trump alitangaza kuwa mzozo huo hatimaye umefikia tamati, akiwashukuru watu aliowaita "wenye vipaji vikubwa” kwa kusaidia kufanikisha juhudi za kidiplomasia.
"Tumefanikisha hilo kupitia msaada wa watu wenye vipaji vikubwa ambao wamesaidia kusuluhisha vita vilivyokuwa vikiendelea kwa miaka mingi kati ya Rwanda na Congo. Na nadhani tumeweza. Uamini usiamini, nadhani tumeweza," alisema Trump.
Soma pia: Ramaphosa: Kuimarisha uhusiano na US ni kipaumbele chetu
Matamshi hayo yameibua hisia tofauti. Wakati baadhi ya watu wanayaona kama ishara mpya ya nia ya Marekani kushiriki katika kudumisha amani barani Afrika, wengine wanaona kauli hiyo kama ya pupa, ikizingatiwa kuwa juhudi za kusuluhisha mzozo wa DRC zimekuwa zikifanywa kwa muda mrefu na jumuiya za kikanda kama SADC.
Rais Ramaphosa, kwa upande wake, alikiri mchango wa Marekani lakini akaweka msisitizo kwa juhudi za ndani za bara la Afrika.
"SADC limekuwa likijitahidi kwa miaka mingi kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hivyo basi, juhudi zote, iwe kutoka ndani ya bara au nje ya bara, ni za thamani sana," alisema Ramaphosa.
Wakongo wa Afrika Kusini wana maoni tofauti
Pamoja na matamshi hayo ya matumaini, si kila raia wa Kongo anaiona Marekani kama mshirika mwaminifu katika juhudi za amani. Kiongozi wa chama cha Wazalendo Afrika Kusini, Ezekiel Ndundu, alikosoa ushirikiano huo akidai kuwa unatoa mianya kwa Marekani kunufaika na rasilimali za Kongo kwa gharama ya raia wake.
Soma pia: Ramaphosa kukutana na Trump White House
"Wakongoman wote wanapenda amani, lakini huwezi ukagawa mali ya nchi yote, eti mtu aje kuchukua mali ya nchi yote eti ndiyo upate amani utabaki na nini wewe?" alihoji.
Msimamo huo uliungwa mkono na mwanachama wa kundi la wazalendo, Bwana Ngalula, ambaye alidai kuwa ushirikiano na Urusi au China ungekuwa na tija zaidi.
"Hii inaonesha Rais Félix Tshisekedi ameshindwa... asimamie wakongo, awe na msimamo mmoja na apiganie wakongomani kama mzalendo wa kwanza nchini DRC," alisisitiza.
Kwa viongozi wa Marekani na Afrika Kusini, suala la mashariki mwa DRC limepewa uzito mkubwa kama la kibinadamu na sio tu la kisiasa. Wanaamini kuwa ushirikiano wa kimataifa na kikanda unaweza kufungua ukurasa mpya wa amani ya kweli na maendeleo kwa ukanda mzima wa Maziwa Makuu.
Lakini maswali yanabaki: Je, matumaini haya mapya ni ya kudumu? Na je, sauti za wananchi zitazingatiwa katika mchakato huu wa kidiplomasia? Muda tu ndiyo utatoa majibu.