Trump, Putin kukutana Ijumaa mjini Anchorage
13 Agosti 2025Ikulu ya White imefahamisha usiku wa kuamkia leo kuwa mkutano huo unaosubiriwa na wengi kati ya Trump na Putin utafanyika katika mji wa Anchorage jimboni Alaska. Msemaji wa rais wa Marekani Karoline Levitt amesema Trump ataelekea kwenye mkutano huo Ijumaa asubuhi na anakusudia kujadiliana na Putin kuhusu vita vya Ukraine.
Leavitt amesema kufikia muda huu, hakuna ratiba yoyote iliyotangazwa kwa kuwa hilo bado linajadiliwa na pande zote, lakini akathibitisha kuwa viongozi hao wawili wamepanga kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja kusini mwa Alaska huko Anchorage ambao ndio mji mkubwa zaidi katika jimbo hilo la kaskazini mwa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani Marco Rubio wamefanya mazungumzo kabla ya mkutano huo wa kilele huko Alaska, na kwa pamoja wameelezea matumaini yao kwamba waliyoyajadili yatafanikiwa, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.
Trump ana matarajio kuwa mkutano huo wa Ijumaa unaweza kusaidia kusitisha vita hivyo, lakini bado kuna mvutano kuhusu suala la kuachia sehemu ya ardhi, jambo linalopingwa mno na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambaye hatohudhuria mkutano huo wa Alaska lakini akasisitiza kuwa hakuna makubaliano yoyote yanayoweza kufanikiwa bila kuishirikisha Ukraine kikamilifu.
Msimamo wa Zelensky na washirika wake wa Ulaya
Zelensky na washirika wake wa Ulaya wanaotarajiwa kuzungumza na Trump leo Jumatano kwa njia ya video, wamesisitiza kuwa mpango wa amani ya kudumu hauwezi kupatikana bila Ukraine katika meza ya mazungumzo, na kwamba makubaliano yoyote ni lazima yazingatie sheria za kimataifa, uhuru wa Ukraine na kuheshimu mipaka ya ardhi yake.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amesema anatumai wataweza kumshawishi Trump kuhusu msimamo wa Ulaya wa kwamba Ukraine haiwezi kushindwa vita hivi na hakuna mwenye haki ya
kuishinikiza Ukraine kusaini makubaliano ya kuachia sehemu ya ardhi yake au kufanya maamuzi ya kujipendekeza.
"Mkutano wa Alaska ni ushindi kwa Putin"
Zelensky amesema kitendo cha rais wa Urusi kukutana na Trump katika ardhi ya Marekani, ni kama ushindi binafsi kwa Putin . Kauli hiyo imeungwa mkono na wachambuzi kadhaa kama Mark Cancian, kanali wa zamani na mshauri mkuu katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa:
"Inasikitisha mno kufanyika mkutano bila Ukraine kuwepo, hilo pekee ni ushindi kwa Putin. Putin haichukulii Ukraine kama nchi yenye uwezo na anataka kuitenga kwenye mijadala. Hilo ni jambo la kukatisha tamaa. Itabidi tuone kitakachotoka kwenye mkutano huo na ikiwa kitamnufaisha Putin."
Hayo yakiarifiwa, mapigano yameendelea kuripotiwa huku wanajeshi wa Urusi wakionekana kusonga mbele zaidi mashariki mwa Ukraine karibu na mji kunakochimbwa makaa ya mawe wa Dobropillia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Putin kuchukua udhibiti kamili wa mkoa wa Ukraine wa Donetsk.
Zelensky amesema pia kuwa anapinga vikali pendekezo la mpango wa usitishwaji mapigano, ambalo Putin anataka Ukraine iachie asilimia 30 inayodhibiti katika mkoa wa Donetsk, na kwamba hatoviondoa pia vikosi vyake katika jimbo la Donbas. Aidha, jeshi la Ukraine limesema limepata mafanikio kidogo katika eneo la kusini-mashariki la Sumy kwa kuvikomboa vijiji viwili kutoka mikononi mwa Urusi.
//DPA, AP, Reuters, AFP