Trump, White House wakalia kuti kavu sakata la Epstein
23 Julai 2025Rais Donald Trump na Ikulu ya Marekani wamejipata katika harakati za dharura za kujaribu kuuzima moto wa kisiasa unaochochewa na taarifa kuhusu Jeffrey Epstein, mtuhumiwa wa ulanguzi wa kingono aliyefariki kwa kujinyonga gerezani mwaka 2019.
Wafuasi wa vuguvugu la MAGA (Make America Great Again) sasa wanamshinikiza Trump atimize ahadi za uwazi kuhusu sakata hilo.
Kwa miaka mingi, Trump na washirika wake walinufaika kisiasa kupitia nadharia za njama zilizoimarisha msingi wa wafuasi wake. Lakini kwa sasa, amejiweka katika nafasi isiyo ya kawaida: kujaribu kuuzima moto wa nadharia hizo hizo ambazo hapo awali ziliwapa nguvu.
Sakata hilo limechochewa upya baada ya utawala wa Trump kufuta uamuzi wa awali wa kutoa hadharani nyaraka za kesi ya Epstein, ambazo awali zilitangazwa kuwa na "ufichuzi mkubwa.” Uamuzi huo wa ghafla umewakasirisha hata baadhi ya wafuasi waaminifu zaidi wa Trump.
Ikulu ya White House yachunguza aatua mpya
Kwa mujibu wa maafisa wawili wa Ikulu, Trump na washauri wake wanatafakari hatua kadhaa za haraka: kufungua baadhi ya nyaraka mpya, kumteua mwendesha mashtaka maalum, na kutangaza maagizo ya kiutendaji yanayolenga vita dhidi ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Aidha, Trump amekuwa akiwahimiza wanaharakati wa MAGA kupunguza mashambulizi ya maneno dhidi ya Ikulu kuhusu sakata hilo.
Suala hili limebainisha mgawanyiko wa ndani katika kundi la kisiasa la Trump na linapima uwezo wake wa kudhibiti mwelekeo wa mazungumzo ya kisiasa miongoni mwa wafuasi wake.
Kwa sasa, baadhi ya wafuasi wamesikitishwa pia na msimamo wa Marekani kuhusu mashambulizi dhidi ya Iran, msaada kwa Ukraine, na udhaifu unaoshukiwa katika msimamo wa Trump kuhusu uhamiaji.
Ripoti ya Wizara ya Sheria iliyotolewa wiki iliyopita ilisema hakuna "orodha ya wateja” wa Epstein yenye ushahidi wa kuvutia, wala dalili kwamba alihusika na vitendo vya kumtishia mtu au kumtega mtu mashuhuri. Pia ilithibitisha kuwa kifo chake kilitokana na kujiua, si shambulizi la makusudi.
Trump, aliyemfahamu Epstein tangu miaka ya 1990, alitajwa katika kesi ya Ghislaine Maxwell – mshirika wa karibu wa Epstein – kuwa aliwahi kupanda ndege binafsi ya mfanyabiashara huyo. Ingawa Trump amekana kuwa alishawahi kupanda ndege hiyo, historia hiyo inazidi kumwekea ugumu wa kujinasua kisiasa.
Trump amkingia kifua mwanasheria mkuu na kuwataka wafuasi wasahau
Trump amejitokeza kumtetea Mwanasheria Mkuu Pam Bondi, ambaye amekosolewa kwa kuashiria awali kuwa kulikuwa na orodha ya wateja wa Epstein. Baadhi ya wafuasi wanataka ajiuzulu, lakini Trump amesisitiza kuwa haoni sababu ya sakata hilo kuendelea kupewa uzito.
"Sielewi kwa nini watu bado wanaendelea kulizungumzia suala la Jeffrey Epstein,” alisema Trump kwa waandishi wa habari. "Ni suala la kusikitisha, lakini pia linachosha. Halina maana yoyote sasa.”
Bondi, alipoulizwa kama anatarajia kuendelea na kazi yake, alisema: "Nitakuwa hapa kwa muda ambao rais ananitaka – na naamini amefafanua hilo wazi kabisa.”
Hata hivyo, mvutano bado upo. Ingawa baadhi ya sauti maarufu kama Charlie Kirk wameanza kurudi nyuma baada ya kushawishiwa na Trump, wengine – hasa katika vyombo vya habari huru na podcast maarufu kama Joe Rogan, Theo Von na Tim Dillon – hawajaacha kuzungumzia suala hilo.
Angelo Carusone, rais wa kundi la uangalizi wa habari la Media Matters for America, alisema: "Inaonekana Trump amepoteza mwelekeo wa matakwa ya wafuasi waliomweka madarakani.”
Wakati huo huo, baadhi ya wanasiasa wa Republican wameendelea kushinikiza uwazi. Spika wa Bunge, Mike Johnson, ameitaka Wizara ya Sheria kutoa nyaraka zaidi.
Mbunge Lauren Boebert aliandika kwenye mtandao wa X: "Tunastahili kujua ukweli kuhusu mafaili ya Epstein. Niko tayari kwa Mwendesha Mashtaka Maalum kulichunguza hili.”
Katika hali hii ya kisiasa isiyotabirika, Trump analazimika kusawazisha kati ya kulinda sura ya utawala wake na kuepuka kupoteza imani ya wafuasi waliomuweka madarakani.