Trump kuzungumza na Putin, Zelensky
19 Mei 2025Kupitia ujumbe wake wa mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki, Trump alisema alikuwa anatazamia mazungumzo yake na viongozi hao wawili siku ya Jumatatu (Mei 19) yangelikuwa na manufaa makubwa kuelekea usitishaji mapigano.
Akiita siku hiyo kuwa "Jumatatu yenye matunda", Trump alisema juhudi zake za upatanishi zingelihusisha pia mazungumzo na viongozi wa Muungano wa Kijeshi wa NATO.
Soma zaidi:Trump kuzungumza na Putin kuhusu usitishaji mapigano Ukraine
Wadadisi wa mambo wanasema mazungumzo hayo ni kipimo kikubwa kwa heshima ya Trump kama mfikiaji mapatano kwa haraka, ambaye amekuwa akijisifia kuwa na uwezo wa kupata mkataba wa amani kati ya Urusi na Ukraine tangu hata hajaingia Ikulu ya White House mapema mwaka huu.
Rais huyo kutokea chama cha Republican anategemea zaidi haiba yake na historia yake binafsi na Putin vinatosha kukiuka vigingi vyote vinavyouzunguka mzozo huo.
"Hisia zake ni kwamba kama akiweza kuzungumza na simu Rais Putin ataweza kuweka sawa mambo yaliyoonesha vikwazo kwenye mazungumzo ya awali ya ngazi za chini." Alisema mshauri wake maalum, Steve Witkoff.
Ikulu ya Urusi, Kremlin, imethibitisha kuwa Rais Putin atazungumza kwa njia ya simu na Trump majira ya saa 11:00 jioni ya leo, kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo, RIA.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema mazungumzo ya viongozi hao wawili yatajikita kwenye matokeo ya majadiliano kati ya Moscow na Kiev yaliyofanyika mjini Istanbul, Uturuki, wiki iliyopita.
Urusi yatwaa vijiji zaidi vya Ukraine
Haya yaliripotiwa wakati wizara ya ulinzi ya Urusi ikisema vikosi vyake vilikuwa vimechukuwa udhibiti wa kijiji cha Novoolenivka kilicho kwenye mkoa wa mashariki mwa Ukraine wa Donetsk.
Shirika la habari la RIA liliinukuu wizara hiyo ikisema kuwa wanajeshi wa Urusi wametwaa pia kijiji chengine cha Marine kwenye mkoa wa kaskazini wa Sumy.
Soma zaidi: Zelensky akutana na viongozi wa Marekani, EU mjini Rome kabla ya simu ya Trump na Putin
Urusi imekuwa ikisonga mbele kwenye eneo la mashariki mwa Ukraine, ambalo ni ukanda wa viwanda, tangu ilipoanza uvamizi wake mnamo mwezi Februari 2022, lakini ni katika siku za karibuni tu ndipo imekuwa ikisonga mbele kuelekea mkoa wa Sumy, baada ya kufanikiwa kuvifurusha vikosi vya Ukraine kwenye mkoa wake wa Kursk.
Haikufahamika kwa kiasi gani hatua hizi za za kijeshi zingeliyaathiri mazungumzo kati ya Trump, Putin na Zelensky, hasa ikizingatiwa kuwa daima msimamo wa Zelensky ni kwamba Putin haaminiki hata kidogo panapokuja suala la kupatikana kwa amani ya kudumu kati ya pande hizo mbili.
Vyanzo: AP, Reuters