Trump kusaini mpango wa bajeti, kutangaza hali ya dharura
15 Februari 2019Muswada wa bajeti ambao Rais Trump amesema atautia saini, na ambao umepitishwa kwa kura nyingi katika mabaraza yote ya bunge unajumuisha kiasi cha dola bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa vizuizi katika mpaka baina ya Marekani na Mexico, kiwango hicho kikiwa chini kabisa ya kile kilichotakiwa na Donald Trump cha dola bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta katika mpaka huo.
Katika Baraza la Wawakilishi linalodhibitiwa na wabunge chama cha Democratic, muswada huo ulipitishwa kwa kura 300 za ndio dhidi ya 128 za hapana, na katika Baraza la Seneti ambako chama cha Republican kina viti vingi, liliungwa mkono na maseneta 83, huku 13 wakiupinga.
Baada ya maamuzi hayo ya bungeni, Ikulu ya Marekani mjini Washington ilithibitisha kwamba Rais Trump atauidhinishwa muswada huo wa bajeti kuwa sheria, huku ikiongeza kuwa atachukua hatua binafsi za kutafuta fedha za kuujenga ukuta mpakani, ambao ni mojawapo ya ahadi kuu za kampeni yake.
Warepublican wagawanyika kuhusu hali ya dharura
Ingawa wapo baadhi ya wabunge kutoka chama cha Trump cha Republican wanaotilia shaka uhalali wa kisheria wa azma yake ya kutangaza hali ya hatari mpakani, wengine, kama Kay Granger kutoka jimbo la Texas, wamemuunga mkono.
''Rais yuko sahihi, huu ni mgogoro ambao tunapaswa kuupatia ufumbuzi kwa manufaa ya wamarekani na wote wanaokuja huku,'' amesema Bi Granger, na kuongeza kuwa ingawa muswada huu ni mdogo mno kuweza kukidhi mahitaji, utawapa maafisa wa usalama wa mpaka nyenzo wanazozihitaji ''kupambana na kitisho kinachotukabili.''
Dalili za mvutano mpya na Wademocrat
Lakini viongozi wa chama cha Demokratic Bungeni, Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi na kiongozi wa walio wachache katika Baraza la Seneti Chuck Schumer, wameonya, kwamba ikiwa Trump atatangaza hali ya hatari, itakuwa hatua inayokwenda kinyume cha sheria, na ambayo ni matumizi mabaya ya madaraka. Mbunge wa chama hicho kutoka jimbo la Florida, Debbie Wasserman-Schultz amesema hatua hiyo wataipinga.
''Ikiwa rais huyu anataka kulihujumu jeshi letu kwa ujanjajanja wa kidikteta, atapaswa kufanya hivyo tu kwa njia inayopita bungeni. Nawaasa wenzangu kuunga mkono muswada huu na kukataa uongo wa Trump wa hali ya dharura mpakani.''
Rais Trump anatarajiwa kutoa tamko baadaye leo, akitazamiwa kutangaza fuko la dola bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta mpakani, ambazo zinajumuisha kiasi kilichoidhinishwa na bunge, na fungu jingine ambalo ataliamua kupitia agizo la rais.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, dpae
Mhariri: Josephat Charo