Trump kukutana na Zelensky kuujadili mzozo wa Ukraine
18 Agosti 2025Rais Zelensky anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo katika Ikulu ya Marekani, White House siku chache baada ya Rais Trump kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin huko Alaska siku ya Ijumaa, mkutano ambao uliashiria kurejea kwa Putin katika jukwaa la kimataifa baada ya kujitenga kwa muda na nchi za Magharibi.
Katika juhudi za kuupatia ufumbuzi mzozo kati ya Urusi na Ukraine, Zelensky atasindikizwa na viongozi wa Ulaya akiwemo Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Rais wa Halshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte.
Shinikizo liongezwe kwa Urusi
Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani, Johann Wadephul ametoa wito wa kuongezwa shinikizo kwa Urusi na kuhakikisha usalama kwa Ukraine katika siku zijazo, ili kuilazimisha Urusi kuelekea katika kupatikana amani ya haki na ya kudumu. Akizungumza Jumatatu na waandishi habari, Wadephul amesema pengine sio kukuza mambo kusema kwamba ulimwengu wote unaitazama Marekani.
''Hakikisho thabiti la usalama ni msingi wa amani ya haki nchini Ukraine, kwa sababu hata baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kupatikana amani, Ukraine inapaswa kuwa na uwezo wa kujilinda yenyewe ipasavyo,'' alifafanua Wadephul. Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani amesisitiza pia kuhusu kuongezwa kwa msaada wa Ukraine.
Siku ya Jumapili, viongozi wa Ulaya akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer walikutana kabla ya mkutano wa leo wa Trump na Zelensky, na kusisitiza kwamba mazungumzo yoyote ya kikanda yatalazimika kuijumuisha Ukraine moja kwa moja.
Huku hayo yakijiri, China imezitolea wito pande zote zinazohusika katika mazungumzo ya amani mjini Washington yenye lengo la kuvimaliza vita vya Urusi nchini Ukraine, kufikia makubaliano ''haraka iwezekanavyo''. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning amewaambia waandishi habari Jumatatu kuwa wana matumaini pande zote na wadau watashiriki katika mazungumzo ya amani kwa wakati na kufikia makubaliano ya amani ya haki, ya kudumu, yenye tija na yanayokubalika kwa pande zote.
Watu 20 wauawa Kharkiv
Aidha, katika uwanja wa mapambano, watu wapatao watano wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa katika shambulizi la anga la Urusi kwenye mji wa Kharkiv uliopo mashariki mwa Ukraine. Meya wa Kharkiv, Ihor Terekhov amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram kuwa mauaji hayo yametokea wakati ambapo Urusi inaendeleza kampeni yake kuripua mabomu na kufanya mashambulizi nchini humo. Akizungumza mapema Jumatatu, Terekhov amesema ndege za kivita za Urusi zilishambulia jengo la makaazi lenye ghorofa nyingi.
Katika hatua nyingine, Gavana wa Jimbo la Zaporizhzhya, Ivan Fedorov amesema roketi pia ziliushambulia mji huo Jumatatu asubuhi, zikiilenga miundombinu ya mijini. Katika shambulizi hilo watu sita walijeruhiwa.
(AFP, DPA, AP, Reuters)