Trump kukutana na Putin huko Alaska Ijumaa
15 Agosti 2025Rais Donald Trump wa Marekani na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin,wanakutana hii leo katika kambi ya kijeshi huko Alaska.
Mkutano huo unatajwa kuwa unaweza kutoa maamuzi na mustakabali wa vita vya Ukraine.
Hii ni kwa mara ya kwanza kwa Rais Putin kuikanyaga ardhi hiyo ya Marekani tangu alipoamuru uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022, vita ambavyo vimeyagharimu maisha ya maelfu ya watu na kufanya uharibifu mkubwa.
Kuelekea mkutano huu wa hii leo, Trump amesema anaamini kwamba Putin yuko tayari kufikia makubaliano:
''Nadhani Rais Putin angependa kuona makubaliano. Nadhani kama nisingekuwa rais, angeitwaa Ukraine yote. Ni vita ambavyo havikupaswa kutokea kamwe. Kama nisingekuwa rais, kwa maoni yangu, angelikuwa tayari kuchukua hatua hizo, kuichukua Ukraine yote. Lakini mimi ni rais na hawezi kucheza na mimi." amesema Trump.
Hata hivyo, Ukraine na washirika wake wa Ulaya wana wasiwasi juu ya makubaliano yanayoweza kufikiwa katika mkutano huo, ikiwa ni pamoja na kuilazimisha Ukraine kukabidhi sehemu ya ardhi yake kwa Urusi ili kuvimaliza vita.