Trump azikosoa Israel na Iran kwa kushambuliana
24 Juni 2025Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema utekelezaji wa makubaliano ya amani kati ya Iran na Israel umeanza rasmi.
Hata hivyo, Trump amezilaumu pande zote mbili kwa kukiuka usitishaji wa mapigano, akieleza kuwa amekasirishwa na hatua zilizochukuliwa na mataifa yote mawili za kushambuliana tena muda mfupi baada ya kutangazwa kwa makubaliano hayo hapo jana.
"Wote wamekiuka makubaliano — Israel pia imekiuka. Mara tu baada ya kufikiwa kwa makubaliano, Israel ilirusha makombora mengi kwa kiwango ambacho sijawahi kushuhudia hapo awali. Sijafurahishwa na Israel. Unajua, ninaposema mambo yako sawa na kwamba sasa mna saa 12 kabla ya utekelezaji kuanza, hupaswi kutumia saa ya kwanza kurusha makombora yote uliyonayo. Kwa hiyo, haikunifurahisha. Lakini pia, sijafurahishwa na Iran."
Ofisi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu imesema Israel, imesitisha kufanya mashambulizi zaidi baada ya kiongozi huyo wa Israel kuzungumza na rais Donald Trump.
Rais Trump akizungumza hii leo kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa Nato,nchini Uholanzi, pia amesema hataki kuona mageuzi ya kiutawala nchini Iran ambayo yanaweza kusababisha machafuko.