Trump awakaribisha White House marais 5 wa Afrika
10 Julai 2025Marais hao waliopokelewa mjini Washington ni kutoka Liberia, Senegal, Gabon, Mauritania na Guinea Bissau. Kwenye kikao hicho masuala kadhaa yamegusiwa ikiwemo ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi, usalama, miundombinu na demokrasia. Mkutano huo pia umekuja katika wakati ambapo rais Trump amefuta msaada kwa mataifa mengi ya Afrika, hatua ambayo imeanza kusababisha athari kwenye bara hilo.
Kwa mujibu wa Ikulu ya White House, mazungumzo hayo kati ya rais wa Marekani Donald Trump na marais hao kutoka nchi tano za Afrika Magharibi na zenye utajiri wa madini yalilenga kwanza kukabiliana na ushawishi wa Urusi na China barani Afrika lakini pia kujadiliana kuhusu masuala ya usalama, biashara na uwekezaji.
Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Trump aliashiria dhumuni la mialiko hiyo akiwaeleza waandishi wa habari kuwa amewapokea marais kutoka nchi zenye ardhi yenye thamani, madini, mafuta na watu wema, huku akiongeza kuwa kuna fursa kubwa za kiuchumi barani Afrika na kwamba analenga kuzidisha ushiriki wa Marekani katika bara hilo.
Marais hao wamwagia sifa Trump na kunadi nchi zao
Walipopewa nafasi ya kuzungumza viongozi hao wa Afrika ikiwa ni pamoja na rais wa Mauritania Mohamed Ould Cheikh El Ghazouani, Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, rais wa Gabon Brice Clotaire Oligui Nguema, Umaro Sissoco Embalo wa Guinea Bissau walimwagia sifa rais Donald Trump huku kila mmoja akinadi kuwa nchi yake inazo rasilimali adimu.
Hata hivyo, rais wa Liberia Joseph Boakai alisisitiza kuwa nchi yake ingependa kushirikiana na Marekani hasa katika masuala ya amani na usalama. Rais Boakai alipomaliza kuzungumza, Trump alionekana kushangazwa na lafudhi yake nzuri ya kiingereza huku akimuuliza ni wapi alipojifunzia.
Mbali na mazungumzo hayo ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Marekani na mataifa hayo ya Afrika, Gazeti la Wall Street limeripoti kuwa Washington ilijaribu pia kuwashawishi marais hao kuwapokea watu wanaofurushwa nchini Marekani.
Trump amerejea madarakani katika muhula wake wa pili akiwa na diplomasia inayoweza kutafsiriwa kama "miamala", huku akitilia umuhimu mkubwa kwenye suala la madini hasa katika mazungumzo na mataifa mengi ya kigeni, mfano Ukraine au kwenye makubaliano ya amani kati ya Rwanda na DRC.
Utawala wa Trump unaonekana kuachana na mfumo wa "misaada ya kigeni unaotegemea hisani" na kuanzisha ule wa ushirikiano na unaodhihirisha kuwa mataifa mengine yanao "uwezo wa kujisaidia yenyewe." Hata hivyo utafiti uliochapishwa katika jarida la Lancet unaonyesha kuwa mabadiliko hayo ya Trump yatasababisha vifo zaidi ya milioni 14 duniani kote wakiwemo watoto milioni 4.5 ifikapo mwaka 2030.
(Chanzo: AFP)