Trump atoa ‘onyo la mwisho’ kwa Hamas kuhusu mateka
7 Septemba 2025Kupitia ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema: "Waisraeli wamekubali masharti yangu. Ni wakati wa Hamas pia kukubali. Nimewaonya kuhusu matokeo ya kutoafiki. Hili ndilo onyo langu la mwisho.”
Mnamo Machi, Trump aliwahi kutoa kauli kama hiyo baada ya kukutana na mateka waliokuwa wameachiliwa, akidai Hamas ikishindwa kuwaachia wengine wote na kukabidhi miili ya waliokufa, "basi mambo yamekwisha kwao.”
Mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023 yalipelekea watu 1,219 kuuawa nchini Israel na wengine 251 kuchukuliwa mateka. Jeshi la Israel linasema 25 kati yao tayari wamefariki, huku 47 bado wakiaminika kushikiliwa Gaza.
Trump pia alisema Marekani ipo "katika mazungumzo ya kina na Hamas” lakini akaonya kwamba ikiwa kundi hilo halitatoa mateka wote, "itakuwa mbaya sana kwao.”
Mashambulizi mapya Gaza
Wakati Trump akitoa onyo hilo, jeshi la Israel lilithibitisha kubomoa jengo refu la makazi mjini Gaza City Jumapili, la tatu kwa siku tatu mfululizo, saa chache baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutangaza kuimarishwa kwa operesheni za kijeshi.
Jeshi lilisema jengo la Al-Roya lilitumika na Hamas kufuatilia harakati za wanajeshi, madai ambayo Hamas imekanusha. Hospitali ya Al-Quds imeripoti kwamba mtu mmoja aliuwawa.
Mashuhuda walisema mlipuko ulioangusha jengo hilo "ulihisi kama tetemeko la ardhi” na kwamba wakaazi wanaishi kwa hofu kubwa.
Netanyahu alisema zaidi ya wakaazi 100,000 tayari wameondoka Gaza City, akiituhumu Hamas kwa kuzuia uhamishaji na kuwatumia raia kama "ngao za kibinadamu.”
Hata hivyo, wakaazi kama Mustafa al-Jamal walisema hawana pa kwenda: "Maeneo tunayotakiwa kuhamia pia yamepigwa mabomu. Hatuna pesa, nyumba, wala chakula.”
Sauti tofauti Israel
Mashambulizi haya yamechochea mijadala ndani ya Israel. Waandamanaji walijitokeza mitaani Jumamosi wakiitaka serikali kuachana na mpango wake wa kuiteka Gaza City, wakihofia hatma ya mateka na wanajeshi.
"Nimehuzunishwa kuona jeshi linaiteka Gaza sasa hivi — kwa mateka, kwa wanajeshi, na kwa raia, hivi ni vita vya kisiasa,” alisema Edith mwandamanaji ambaye aligoma kutoa jina lake la pili.
Kiongozi wa upinzani Yair Lapid naye aliishutumu serikali ya Netanyahu kwa, kile alichokiita "kuzorotesha juhudi za kidiplomasia.” Alisema: "Kuna mpango wa mateka mezani. Unaweza kufanyika, lazima ufanyike.”
Lapid alifichua kuwa majadiliano ya wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar yamepiga hatua, lakini Israel haijajibu mapendekezo yao ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa makadirio ya Israel, bado mateka 48 wako mikononi mwa Hamas, takribani 20 kati yao wakiwa hai na wengi wakiaminika kufichwa kwenye mitaro ya Gaza City.
Maandamano Brussels
Nje ya Mashariki ya Kati, mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, ulishuhudia maandamano makubwa Jumapili ambapo maelfu waliandamana kuwaunga mkono Wapalestina. Polisi walisema walikuwepo takribani waandamanaji 70,000, huku waandaaji wakisema idadi ilifika 120,000.
Wengi walivaa nguo nyekundu na kubeba kadi nyekundu, wakitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali zaidi dhidi ya Israel ili kulinda raia wa Gaza.
Mmoja wa waandamanaji, Ismet Gumusboga mwenye umri wa miaka 60, alisema: "Wengine waliota kuanguka kwa Ukuta wa Berlin. Mimi naota kuhusu taifa la Palestina huru.”
Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Maxime Prevot alisema wiki iliyopita kwamba Umoja wa Ulaya "unapoteza uhalali” kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya vita vya Gaza.
Ubelgiji imetangaza kwamba itatambua taifa la Palestina kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi huu na tayari imeweka vikwazo vipya dhidi ya Israel.
Vifo na mateso vinaendelea
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas, watu wasiopungua 64,368 wameuawa Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel, wengi wao wakiwa raia. Umoja wa Mataifa unasema takwimu hizo zinaaminika.
Israel, kwa upande wake, inasema inalenga miundombinu ya Hamas na haikusudii raia, ikishikilia kwamba kundi hilo ndilo linahatarisha maisha ya watu kwa kujificha miongoni mwao.
Kwa upande wa Marekani, Trump amejitanabaisha kama mpatanishi mkuu, lakini onyo lake la hivi karibuni linaweza kuongeza shinikizo kwa Hamas na pia kugawanya maoni kimataifa kuhusu njia bora ya kumaliza vita.
Hamas imesema Jumapili iko tayari "kuketi mara moja mezani kwa mazungumzo” kufuatia kile ilichoeleza kama "baadhi ya mawazo kutoka upande wa Marekani yanayolenga kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.”
Hali Gaza inabaki kuwa ya hatari, huku raia wakiendelea kukimbia bila usalama wa kudumu na matarajio ya makubaliano yakisalia dhaifu.
Chanzo: AFPE, DPAE, RTRE