Trump atangaza kukutana na Putin siku za usoni
17 Februari 2025Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa hakuna muda uliowekwa, lakini inaweza kuwa katika siku za usoni.
Kauli ya Trump imetolewa saa chache kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kuanza ziara yake katika mji mkuu wa Saudi Arabia- Riyadh, ambako atakutana na viongozi wa Urusi na kujadili namna ya kuumaliza mzozo wa Ukraine ambao unakaribia kutimiza miaka mitatu.
Akizungumza na waandishi wa habari Trumpa amesema timu yake imekuwa ikizungumza "kwa muda mrefu na kwa bidii" na maafisa wa Urusi, akiwemo mjumbe wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati Steve Witkoff ambaye kulingana na Trump alikutana na Putin hivi majuzi kwa takriban masaa matatu.
Soma pia: Viongozi wa Ulaya watakutana Paris kujadili usalama wa Ukraine
"Nadhani anataka kuacha vita, na ikiwa angeendelea, basi hilo lingenisababishia tatizo kubwa," Trump alijibu akimzungumzia Putin, lakini alipoulizwa ikiwa anaamini Putin anataka kuchukua udhibiti wa Ukraine nzima, Trump alisema: "Hilo lilikuwa swali langu kwake".
Rais huyo wa Marekani aliendelea kusema: "Nadhani Putin anataka kuvimaliza vita, na wote, (yaani Zelensky) wanataka kuvimaliza haraka".
Mataifa ya Ulaya yamekuwa yakikosoa harakati za Marekani za kuongoza mazungumzo ya amani bila kushirikishwa. Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema nchi za Ulaya na Ukraine zitajumuishwa kwa wakati muafaka kwenye mchakato huo.
Zelensky: Urusi inajiandaa kupambana na NATO
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema siku ya Jumapili kuwa anaamini kwamba Urusi inajiandaa "kuanzisha vita" dhidi ya Jumuiya ya kujihami ya NATO iliyodhoofika, iwapo Trump atapunguza uungaji mkono wa Marekani kwa muungano huo wa kijeshi.
Hata hivyo Trump ameonekana kupuuzilia mbali matamshi ya Zelensky, akisema "hana wasiwasi hata kidogo" kuhusu kauli ya kiongozi huyo wa Ukraine. Trump aliahidi kuwa atakaporejea madarakani ataumaliza mzozo wa Ukraine kwa muda wa siku moja, lakini Rubio amesisitiza kuwa "haitakuwa rahisi" kuutatua mzozo huo tata, wa muda mrefu na wa umwagaji damu.
Soma pia: Vance asema Marekani inatafuta "amani ya kudumu" kwa Ukraine
"Mchakato kuelekea amani sio jambo la mkutano mmoja," mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani alisema katika mahojiano na shirika la habari la CBS kando ya Mkutano wa Usalama wa Munich uliomalizika Jumapili.
Katika mahojiano na shirika la habari la NBC siku ya Jumapili, Rais Zelensky alisema Putin ni mwongo mkubwa na hawezi kuaminiwa kama mshirika wa mazungumzo.
Rubio alijibu kwa kusema: "Sidhani katika siasa za kijiografia, mtu yeyote anapaswa kumwamini mtu yeyote, wiki na siku chache zijazo ndizo zitaamua ikiwa Putin analitia maanani au la suala la mazungumzo ya amani."
Vyanzo: AFP/DPA