Trump atangaza kuiondolea vikwazo vyote Syria
14 Mei 2025Akizungumza mjini Riyadh, kiongozi huyo wa Marekani pia ameahidi kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Syria akisema kwamba sasa ni wakati wa nchi hiyo kusonga mbele na kuipa nafasi muhimu ya kuufufua uchumi wake ulioporomoka kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi.
Ameeleza kuwa vikwazo dhidi ya Syria vimetimiza malengo yake na hivyo havihitajiki tena.
Soma pia: Trump awatolea wito Putin na Zelensky kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano
Tangazo la Trump kuiondolea Syria vikwazo linaashiria mabadiliko makubwa katika sera ya muda mrefu ya Washington kuhusu Syria, ambapo vikwazo viliilenga serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad, na nchi hiyo kwa ujumla kutokana na visa vya ukandamizaji wa upinzani na ukiukwaji wa haki za binadamu katika muda wa karibu miaka 14.
Akitoka Riyadh, Rais huyo wa Marekani atasafiri kuelekea Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo tayari imeahidi kuwekeza dola trilioni 1.4 nchini Marekani katika kipindi cha muongo mmoja ujao.