Trump atangaza kuiondolea vikwazo vyote Syria
14 Mei 2025Rais Donald Trump amesema kuwa Marekani haina mshirika wa karibu zaidi kuliko Saudi Arabia wakati wa ziara yake ya kwanza nje ya nchi – ziara katika mataifa ya Ghuba inayolenga zaidi kuimarisha uwekezaji.
Akizungumza mjini Riyadh, kiongozi huyo wa Marekani pia ameahidi kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Syria akisema kwamba sasa ni wakati wa nchi hiyo kusonga mbele na kuipa nafasi muhimu ya kuufufua uchumi wake ulioporomoka kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi.
Soma pia: Mataifa ya Kiarabu yatazamia biashara na Marekani licha ya vita Gaza
Ameeleza kuwa vikwazo dhidi ya Syria vimetimiza malengo yake na hivyo havihitajiki tena.
Tangazo la Trump kuiondolea Syria vikwazo linaashiria mabadiliko makubwa katika sera ya muda mrefu ya Washington kuhusu Syria, ambapo vikwazo viliilenga serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani Bashar al-Assad, na nchi hiyo kwa ujumla kutokana na visa vya ukandamizaji wa upinzani na ukiukwaji wa haki za binadamu katika muda wa karibu miaka 14.
Trump kukutana na kiongozi wa mpito wa Syria
Afisa mmoja katika Ikulu ya White House amesema Trump anatarajiwa kukutana na kiongozi wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa leo Jumatano nchini Saudia Arabia, mkutano kati ya kiongozi huyo wa Marekani na kamanda wa zamani wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda aliyechukua madaraka baada ya Bashar al-Assad kuondolewa madarakani.
Vyanzo viwili kutoka ofisi ya kiongozi huyo wa Syria vimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba, Trump na al-Sharaa watakutana leo asubuhi.
Soma pia: Marekani na Saudi Arabia zatia saini makubaliano ya uchumi, ulinzi
Trump amechukua uamuzi wa kuiondolea Syria vikwazo baada ya majadiliano na Mohamed bin Salman na Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan, ambao wote wawili wameunga mkono kuondolewa kwa vikwazo hivyo.
Siku ya kwanza ya ziara ya Trump imeshuhudia pia Marekani na Saudi Arabia zikitia saini makubaliano ya silaha yenye thamani ya dola bilioni 142, pamoja na uwekezaji mwingine ambao mrithi wa kiti cha ufalme Mohammed bin Salman ameeleza kuwa, unaweza kufika hadi thamani ya dola trilioni moja.
Trump pia aliifanya Saudi Arabia kuwa kituo chake cha kwanza cha kigeni wakati wa muhula wake wa kwanza madarakani mnamo mwaka 2017. Ziara yake ya sasa itajumuisha pia kuzitembelea Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE.
Katika hotuba yake kwenye kongamano la uwekezaji, Trump ameusifu uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia akiutaja kuwa "wenye nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.”
Soma pia: Saudi Arabia yataka Israel ishinikizwe iruhusu misaada Gaza
Amesema, "kuanzia tulipoanza, tumeshuhudia utajiri ukimiminika – na unaendelea kumiminika nchini Marekani.”
Trump anajaribu kuwavutia wawekezaji wa kigeni kuwekeza Marekani ili kukuza uchumi wa taifa hilo, moja kati ya kipaumbele kikuu cha serikali yake katika takriban miezi minne ya muhula wake wa pili.
Akitoka Riyadh, Rais huyo wa Marekani atasafiri kuelekea Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo tayari imeahidi kuwekeza dola trilioni 1.4 nchini Marekani katika kipindi cha muongo mmoja ujao.