Trump atangaza kuachiwa mateka aliyezuiwa na kundi la Iraq
10 Septemba 2025Trump aliandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Truth Social hapo jana Jumanne kwamba Tsurkov ameachiwa na kundi la wanamgambo la Kataeb Hezbollah baada ya kuteswa kwa miezi mingi na sasa yuko katika ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.
Duru ndani ya kundi hilo lenye nguvu kubwa imesema msomi huyo aliachiliwa kuepusha mizozo yoyote nchini Iraq na kuwezesha kuondolewa kwa vikosi vya Marekani.
Kundi la Kataeb Hezbollah halikudai kuhusika na utekaji nyara wa Tsurkov lakini duru hiyo imeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba mwanamama huyo aliachiliwa huru kulingana na masharti, muhimu kati yao ikiwa ni kuwezesha kuondoka kwa majeshi ya Marekani bila mapigano na kuiepushia Iraq migogoro au mapigano yoyote.
Tsurkov aliachiwa huru na hakuna operesheni yoyote ya kijeshi iliyofanywa kumkomboa.