Trump: Wapatanishi wa Marekani waelekea Urusi
13 Machi 2025Kufuatia mazungumzo ya ufanisi na Ukraine kuhusu usitishwaji mapigano, ujumbe wa Marekani uko njiani kuelekea mjini Moscow kwa mujibu wa rais wa Marekani Donald Trump. Trump alisema jana katika ikulu ya mjini Washington katika dhifa ya kukmaribisha waziri mkuu wa Ireland Michael Martin kwamba wana watu wanaoelekea Urusi hivi sasa. Trump alisema mazungumzo na Ukraine mjini Jeddah nchini Saudi Arabia yalikuwa na mafanikio makubwa akiongeza kusema sasa ni wajibu wa Urusi kuchukua hatua.
Siku ya Jumanne ujumbe wa Ukraine ulitangaza utayari wa kukubali mpango wa usitishaji mapigano mara moja kwa kipindi cha siku 30. Marekani ikaanza tena kutuma msaada wake wa kijeshi kwa Ukraine ambao ulikuwa umesitishwa kwa muda.
Mawaziri wa ulinzi wa nchi za Ulaya wajadili Ukraine
Wakati huo huo, mawaziri wa ulinzi wa nchi tano za Ulaya wanachama wa jumuiya ya kujihami NATO walikutana jana mjini Patis, Ufaransa kujadili hakikisho la usalama wa kijeshi kwa Ukraine, pamoja na uwezekano wa kupeleka vikosi vya kudumisha amani, iwapo mkataba wa amani utaafikiwa pamoja na Urusi.
Mawaziri hao wa ulinzi wa Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland na Uingereza, hawakutoa maelezo kuhusu muundo hasa na nguvu ya kikosi hicho kufuatia mazungumzo hayo.
Soma pia: Urusi yapongeza hatua ya Ukraine kuwa tayari kwa mazungumzo ya amani
Waziri wa ulinzi wa Uingereza John Healey amesema katika mkutano na waandishi habari baada ya mkutano huo kwamba Uingereza na Ufaransa zinaongoza kwa pamoja kazi ya kuratibu kuongoza juhudi za kuundwa kikosi hicho cha amani na mipangilio ya hakikisho la usalama kwa Ukraine.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Sébastien Lercornu kwa upande wake alisisitiza kwamba hakikisho la kwanza la usalama kwa Ukraine ni majeshi ya Ukraine. Alisema washirika wanapania kuliimarisha jeshi la Ukraine kwa kipindi kirefu kama walivyofanya tangia mwanzo wa vita. Lercornu alisema hawawezi kuvitaka vikosi vya Ulaya vifanye kazi ya majeshi ya Ukraine. Hata hivyo amedokeza kwamba Ulaya huenda ikatafakari kupeleka vikosi katika mpaka wa Poland na Ukraine. Mawaziri hao wa ulinzi pia walijadili kuongeza juhudi za kupeleka silaha na uratibu bora zaidi kati ya majeshi.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius alisema nchi za Ulaya zinahitaji kufanya juhudi kuulinda usalama wa Ulaya na kuweka kando masilahi ya kitaifa. Ameongeza kusema wanahitaji kununua vifaa vya kijeshi vya viwango vinavyostahili kwa kiwango kikubwa na kwa haraka zaidi kuliko hapo kabla.
Finland kuwa sehemu ya muungano wa kuisaidia Ukraine
Wakati haya yakiarifiwa, Finland imesema itakuwa sehemu ya muungano wa nchi zinazojitolea kwa hiari ambazo huenda zikasaidia kuimarisha usalama wa Ukraine. Waziri wa mambo ya nje wa Finland Elina Valtonen ameiambia Times Radio ya Uingereza jana Jumatano kwamba wao bila shaka ni sehemu ya muungano huo na wanaangalia uwezo walionao kuwasilisha mezani ili kuisaidia Ukraine kujilinda yenyewe.
Awali Jumatano waziri mkuu wa Finland Petteri Orpo alisema Finland ilikuwa inashiriki mazungumzo kuhusu kuundwa kwa muungano wa nchi zilizo tayari kwa hiari kuisaidia Ukraine, lakini akafutilia mbali ushiriki wowote katika tume ya amani nchini Ukraine, akitaja umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa Finland yenyewe karibu na Urusi.
Putin afanya ziara ya kushtukiza Kursk
Wakati haya yakiarifiwa kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine Oleksandr Syrskyi amesema hivi leo kwamba vikosi vya Ukraine vitaendelea kufanya operesheni zake katika eneo la Urusi la Kursk kwa muda mrefu itakavyohitajika na kwamba mapigano yataendelea ndani na nje ya mji wa Sudzha. Kamanda huyo ameongeza kusema vikosi vinasonga mbele katika maeneo ya kimkakati kama inahitajika kwa lengo la kuyaokoa maisha ya wanajeshi. Kwa mujibu wa Syrskyi mapigano yameendelea mjini Sudzha na viunga vyake.
Rais wa Urusi Vladimir Putin pasipo kutarajiwa amekitembelea kituo cha kamandi ya kijeshi mjini Kursk katika eneo la vita kufuatia operesheni ya mafanikio iliyofanywa na vikosi vyake katika eneo la mpaka kati ya Urusi na Ukraine. Chombo cha habari cha serikali ya Urusi TASS kimeripoti jana Jumatatno kwamba Putin aliamuru vikosi vya Urusi viwafurushe wanajeshiw a vikosi vyote vya Ukraine waliobaki mjini Kursk.
Picha za mkutano na mnadhimu mkuu wa jeshi Valery Gerasimov zilimuonesha Putin akiwa amevalia sare za jeshi. Eneo halisi la mkutano halikutajwa. TASS imesema ilikuwa ziara ya kwanza ya Putin katika sehemu hiyo ya uwanja wa vita.
Mnamo Agosti 2024, vikosi vya Ukraine viliivamia Urusi bila kutarajiwa, na hivyo kuvihamishia vita katika himaya ya adui kwa mara ya kwanza. Baada ya vikosi vya Ukraine kuendelea kulishikilia eneo hilo kwa muda mrefu, wamelazimika kurudi nyuma kwa haraka zaidi katika siku za hivi karibuni wakiwa chini ya shinikizo la Urusi.
Siku ya Jumatano, kwa mujibu wa Urusi, wanajeshi wa Urusi waliuteka na kuudhibit mji mkuu wa eneo hilo, Sudzha, ambao ulikuwa uti wa mgongo wa kusonga mbele kwa Ukraine kwa miezi saba. Hata hivyo eneo hilo bado halijasawazishwa kabisa na vikosi vya Ukraine kufukuzwa.