Trump: Putin ana wazimu kuendelea na mashambulizi Ukraine
26 Mei 2025Trump amesema siku zote amekuwa akisema Putin anataka kuidhibiti Ukraine yote kikamilifu na sio tu sehemu ndogo ya taifa hilo, akiongeza kuwa hatua ya Putin itasababisha kusambaratika kwa taifa lake Urusi.
"Sijafurahishwa na anachofanya Putin. Anaua watu wengi sana. Na sijui nini kimemtokea Putin. Nimemjua kwa muda mrefu, tumesikizana sana. lakini anarusha makombora mijini na kuua watu na sipendi kabisa. Sawa? Tuko katikati ya mazungumzo na anarusha makombora Kyiv na miji mingine. Sijapenda hata kidogo," alisema Trump.
Trump: Putin amekuwa mwendawazimu kwa kuendeleza mashambulizi
Rais huyo wa Marekani pia amemkosoa ais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, akisema haitendei haki nchi yake kwa matamshi yake yake aliyosema yanasababisha matatizo na kumuomba ajifunze kukaa kimya. Hadi sasa hakuna majibu yoyote kutoka Ikulu ya Urusi au kutoka kwa Zelensky kuhusu kauli za Trump.
Trump amekuwa akitoa shinikizo kwa Urusi na Ukraine kusitisha vita vyao vilivyodumu miaka mitatu, lakini pande hizo mbili bado zinaendelea kujitenga na hilo huku mapigano yakiendelea na vikosi vya Urusi vikizidi kusonga mbele Mashariki mwa Ukraine.