Trump asema atakutana na Putin hivi karibuni
7 Agosti 2025Rais Donald Trump wa Marekani amesema atakutana na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin ana kwa ana hivi karibuni ili kujadili usitishwaji wa vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Trump amesema mkutano wake na Putin ni matokeo ya mazungumzo yenye tija kubwa yaliyofanyika mjini Moscow kati ya mjumbe wake maalum Steve Witkoff na Rais Putin.
''Na hatujaamua wapi, lakini tulikuwa na mazungumzo mazuri sana na Rais Putin, na kuna nafasi nzuri sana kwamba tunaweza kufikia makubaliano ya mwisho ya kumaliza vita. Safari hiyo ilikuwa ndefu na inaendelea kuwa ndefu, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba kutakuwa na mkutano hivi karibuni." amesema Trump.
Urusi tayari imethibitisha kuhusu mkutano huo huku Rais wa UkraineVolodymyr Zelensky nae ametoa wito wa kukutana ana kwa ana na Putin ili kuzungumza namna ya kuvimaliza vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.