Trump arudi tena katika mkutano wa G7
13 Juni 2025Mkutano wa G7 unaoanza Jumapili katika mji wa Kananaskis, eneo la milima nchini Canada, unawakilisha mkutano mkubwa wa kimataifa katika muhula wa pili wa Trump, anayeongoza katika kuvunja kanuni za kidiplomasia.
Ili kuepuka migogoro, Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, aliweka ajenda yenye mada zisizoleta mizozo, kama vile kujenga minyororo ya usambazaji wa madini muhimu duniani.
Hata hivyo, ajenda hiyo inaweza kubadilika baada ya Israel kuanzisha kampeni kubwa ya kijeshi dhidi ya Iran siku ya Ijumaa, ikidai kuwa ni hatua ya kuzuia mapema harakati za mpango wa kutumia nyuklia unaopangwa na adui wake.
Serikali ya Trump imeungana kwa karibu na Israel, hata kwa kuwalaumu washirika wake wanaoyakosoa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Lakini licha ya Marekani kuiunga mkono Israel wakati wote, Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, alikataa waziwazi mwito wa Trump, ambaye saa machache kabla ya shambulio hilo alikuwa amehimiza juu ya suluhisho la kidiplomasia. Mjumbe wake, Steve Witkoff, alikuwa amepangiwa kuendesha mazungumzo mapya na Iran siku ya Jumapili, wakati mkutano wa G7 unapoanza.
Afisa mmoja wa Canada amesema, haitakuwa rahisi kwa wanachama wa G7 kufikia makubaliano ya tamko la pamoja juu ya masuala yaliyopo. Badala yake, viongozi watatakiwa kuunga mkono "matamko mafupi, yanayolenga zaidi hatua za vitendo."
Chuku dhidi ya Canada
Mara ya mwisho Trump kuhudhuria mkutano wa G7 ulioandaliwa Canada mwaka 2018, aliondoka ghafla na kuchapisha katika mitandao ya kijamii akiteenga Marekani na tamko la pamoja, akimwita Waziri Mkuu wa wakati huo Justin Trudeau "mwongo na dhaifu.”
Chuki kati yao haikuwahi kuisha, na Trump alaporudi madarakani aliwahi kusema kwa kejeli kuwa Canada inapaswa kuwa jimbo la 51 la Marekani.
Kundi la G7, lenye nchi saba kubwa zenye uchumi wa viwanda — Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani — lilianzishwa miaka ya 1970 kwa ajili ya kuratibu sera za uchumi na limeimarika katika kushughulikia pia baadhi ya masuala magumu ya usalama duniani.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, anapanga kuhudhuria mkutano wa G7 na anatarajia kukutana na Trump. Wawili hao waligombana vikali katika Ikulu ya Marekani mnamo Februari, lakini tangu wakati huo Trump ameonyesha kukata tamaa kutokana na ukimya wa Urusi kuhusu juhudi za amani.
Katika hatua muhimu ya kujitenga na waziri wa zamani Trudeau, Carney amemwalika Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi. Uhusiano kati ya Canada na India ulizorota kwa kasi baada ya Trudeau kuituhumu India hadharani kwa kupanga mauaji ya mpinzani wa Sikh nchini Canada.