Trump apuuza uvujishaji wa chat kuhusu mashambulizi Yemen
26 Machi 2025Trump amesema hakuna taarifa za siri zilizovuja kupitia kundi hilo katika mtandao wa mawasiliano wa Signal, na amemtetea mshauri wake mkuu wa masuala ya usalama, Mike Waltz, aliyesababisha tukio hilo.
Mwandishi Jeffrey Goldberg wa jarida la The Atlantic amesema Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, alituma ujumbe kuhusu maeneo ya kushambuliwa, silaha na muda wa mashambulizi yaliyofanyika Machi 15, pamoja na ukosoaji mkubwa dhidi ya washirika wa Ulaya kutoka kwa maafisa wa juu wa Marekani.
Akizungumza na wanahabari, Trump amemshambulia Goldberg akimtaja kuwa "mtu asiyeaminika," na kudai kwamba hakuna anayejali kuhusu taarifa hizo.
Wakati huo huo, mshauri Mike Waltz amekiri kuwajibika kwa kosa hilo, akisema lilisababishwa na kuhifadhi namba ya Goldberg kimakosa kwenye simu yake chini ya jina tofauti.