Trump aondoka mkutano wa G7 baada ya kutoa onyo kwa Iran
17 Juni 2025Trump hakuweka wazi sababu hasa ya kuondoka kwake katika mkutano huo, lakini alizima matumaini ya usitishwaji mapigano, kwa kuwataka watu wa Tehran kuondoka mjini humo na kisha kumokosoa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kupendekeza kuwa usitishwaji wa vita vinavyoendelea kati ya mataifa hayo mawili hasimu unawezekana.
Trump aliandika katika mtandao wake wa kijamii kwamba Iran ilipaswa kutia saini mkataba wa nyuklia uliokuwepo, akisisitiza kuwa kinachotokea sasa ni kitendo cha aibu kuona watu wanaangamia. Ameendelea kusema kwamba Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia, akionya kuwa wakazi wa Tehran wanapaswa kuondoka mara moja mjini humo.
Trump akatisha mkutano wa G7 wakati mzozo wa Israel na Iran ukiongezeka
Hatua ya Trump kuondoka katika mkutano huo ilijiri baada ya rais Macron kuashiria uwepo wa mazungumzo ya amani, akisema pendekezo la usitishwaji wa mapigano kati ya Israel na Iran pamoja na mikutano na majadiliano inafanyika, bila kuweka wazi wanaoendesha juhudi hizo.
Kabla ya kuondoka kwake kundi hilo la nchi saba tajiri kiviwanda G7 linalojumuisha Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Japan na Canada lilitoa taarifa ya pamoja kuunga mkono hatua ya Israel kujilinda na kupinga pia Iran kumiliki silaha za nyuklia. Kundi hilo limeitaja Iran kama chanzo cha kuyumba kwa kanda hiyo ya Mashariki ya Kati.
China yakosoa kauli ya Marekani
Hata hivyo China imemkosoa Trump kwa kauli yake ya kuwataka wakaazi wa Tehran kuondoka makwako akisema kauli kama hizo ni za kichochezi zinazoongeza mafuta kwenye moto. Msemaji wa wizara ya ya kigeni ya China Guo Jiakun, amesema vitisho na uchochezi haviwezi kutuliza hali bali vinachochea zaidi mgogoro kutanuka katika kanda nzima.
Mkutano wa G7 kufunguliwa Canada katikati ya mizozo duniani
Awali Trump aliwahi kusema kwamba Iran inaweza kuwa tayari kwa majadiliano ya kusitisha mpango wake wa nyuklia lakini akasema atalishughulikia suala hilo baada ya kurejea nyumbani kutoka Canada. Hata hivyo kuna wasiwasi kwamba kiongozi huyo wa Marekani huenda akachukua hatua ya kijeshi zaidi inayohofiwa huenda ikatanua mzozo huo.
Kwa trump kuondoka katika mkutano huo kuneonekana kama kizingizi cha kutatua matatizo mengi yanayoikumba dunia kuanzia vita vya Urusi na Ukraine, Israel na Gaza hadi biashara ya kimataifa. Tayari rais huyo wa Marekani alikosoa hatua ya kumuacha nje Rais wa Urusi Vladimir Putin katika mkutano huo licha ya Moscow kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya Kiev.
reuters,ap,afp